Pigo kubwa kwa al-Qaeda Afrika Mashariki
13 Juni 2011
Kwanza aliuawa Osama bin-Laden na sasa ni kiongozi wa al-Qaeda katika Mashariki ya Kati. Marekani imesherehekea kifo cha Fazul Abdullah Mohammed kama pigo kubwa dhidi ya mtandao wa kigaidi. Kwa miaka kadhaa, kiongozi huyo wa ugaidi aliweza kujificha na mara kwa mara alikwepa kukamatwa akitumia majina mavazi tofauti. Safari hii alipigwa risasi na kuuawa, baada ya kusimamishwa kwa bahati tu, kwenye kituo cha ukaguzi barabarani, nchini Somalia. Afisa wa serikali ya Marekani amesema, sasa kundi la al-Qaeda limepoteza kiongozi mwenye ujuzi mkubwa wa kupanga operesheni za mtandao huo.
Ukweli ni kwamba kundi hilo la kigaidi, limedhoofika kutokana na kifo cha Fazul Abdullah Mohammed aliekuwa na umri kama miaka 40. Yeye alikuwa mwerevu, mtaalamu wa compyuta, alizungumza lugha tano kwa ufasaha na yeye ndiye aliepanga shambulio la kwanza kabisa la al-Qaeda. Hata kabla ya mashambulizi ya Septemba 11 mwaka 2001, kundi hilo la kigaidi mnamo mwezi wa Agosti mwaka 1998, lilishambulia kwa wakati mmoja, balozi za Marekani nchini Tanzania na Kenya.
Mashambulio hayo yalisababisha vifo vya takriban watu 240. Kuanzia hapo, Fazul Abdullah Mohammed alikuwa katika orodha ya watu wanaosakwa zaidi.
Kufuatia kifo cha Osama bin-Laden, ilichukuliwa kuwa yeye ndio atakaerithi nafasi yake. Inasemekana kuwa wote wawili walikuwa na heba. Wale waliokuwa karibu nao, wamewaeleza kama watu waliokuwa wema, waliotulia na waliokuwa na vipaji vya kuvutia watu.
Na kwa mtandao wa al-Qaeda, Fazul Abdullah Mohammed alikuwa muhimu sana kwani aliweza kuwavutia wafuasi wapya. Yeye alitayarisha kambi za kutoa mafunzo kwa washambuliaji vijana nchini Somalia na aliweza kuwasadikisha kuwa ni sahihi kujitoa mhanga kwa Mwenyezi Mungu. Sasa, tawi la al-Qaeda katika Mashariki ya Kati limeachwa na pengo.
Lakini mtandao wa al-Qaeda hauna shida ya kupata wafuasi wapya, kwani nchini Somalia kuna maelfu ya wanaume vijana, wasiojua chochote isipokuwa vita na wao wapo tayari kujitoa mhanga.
Mwandishi: Diekhans,Antje,ZPR
Mhariri:Miraji Othman