1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Pigo kwa Guantanamo

5 Juni 2007

Gereza la Guantanamo limepata pigo la kisheria jana juu ya kuwahukumu watuhimiwa wa ugaidi.Hii ni kwa muujibu wa hukumu iliopitishwa jana na Tume ya kijeshi.

Hii ni kwa muujibu wa hukumu ya kusangaza iliopitishwa jana na hakimu wa kijeshi Col.Peter Brownback.Alitupilia mbali mashtaka ya mauaji na mengineo dhidi ya mshtakiwa Omar Kadr-mwanajeshi wa Al Qaeda mwenye umri wa miaka 20.Col.Brownback alidai Tume yake ya kijeshi haina mamlaka ya kisheria kumhukumu Khadr,mzaliwa wa Kanada.

Kiongozi wa mawakili wa washtakiwa wa Jeshi la Marekani Guantanamo, Kanali Dwight Sullivan,alisema hakuna mfungwa aliepitishiwa hukumu ya ‘mpiganaji-adui-aliehalifu sheria” –unlawfully enemy combatant- kama inavyostahiki chini ya sheria za Marekani.

Kwahivyo, aliwaambia maripota jana Tume ya kijeshi ilioundwa na sheria ya Bunge la Marekani (congress) mwaka jana haina msingi wa kisheria kuwahukumu akina Khadr na wafungwa wengineo waliomo korokoroni huko Guantanamo.

Sullivan na wakereketwa wa haki za binadamu wamesema, hukumu iliopitishwa jana na kanali Brownback, haikuamua juu ya uhalali wa serikali ya Marekani wa kuwaweka korokoroni watuhumiwa 380 wa vita dhidi ya ugaidi.

Serikali ya marekani inashikilia ina haki ya kuweka watuhumiwa hao gerezani tena bila mashtaka na Khadr binafsi yadhihirika atasalia Guantanamo huku kuwekwa kwake zaidi huko kunatatanisha kisheria.

Hukumu kamili ya mfungwa wa Guantanamo iliokamilishwa hadi sasa ni ile ya kijana wa miaka 31 wa Ki-australia-David Hicks-maarufu “Mtaliban wa Australia” aliehukumiwa kifungo cha miezi 9 mwezi machi mwaka huu baada ya kuafikiana na upande wa mashtaka.Hivi sasa amewekwa gerezani huko Adelaide,Australia.

Kanali Dwight Sullivan,wakili wa mshtakiwa amesema hukumu aliopitishiwa jana Khadr yaweza ikawa na athari zake kwa Muastralia huyo Hicks.

Sharti la kimsingi kwamba adui-mhalifu-sharia pekee ndie awezae kuhukumiwa huko Guantanamo lilipitishwa na Bunge katika mswada wa Tume ya kijeshi hapo Septemba mwakajana.Lakini, Hakimu wa Tume ya kisheria ya jeshi, Kanali Brownback, aligundua kuwa pale Khadr aliposikilizwa mashtaka yake mara moja tu na mahakama maalumu septemba mwaka 2004 alipewa hadhi ya zamani waliotumiliwa wafungwa –yaani “mpiganaji-adui” na sio “mpiganaji-adui-mhalifu wa sheria.”

Mtuhumiwa mwengine ugaidi,Salim Ahmed Hamdan,raia wa Yemen aliezaliwa 1970,pia alifikishwa mbele ya Tume hiyo ya mahkama hapo jana.Amshtakiwa kutumika tangu kama mlinzi-bodiguard wa Osama bin Laden na kama dereva wake.

Priti Patel,mwanasheria wa kikundi kinachotetea haki za binadamu-amesema mkasa wa Khadr ni pigo kubwa kwa utawala wa rais George Bush.

Wachunguzi wengine wanakubaliana nae ingawa wanabashiri kuwa serikali ya Bush itaendelea na mashtaka dhidi ya Khadr.

Jumana Musa wa Shirika linalotetea wafungwa wa kisiasa na haki za binadamu-Amnesty International- asema matatizo yanaoukumba utawala wa Bush kuhusi jinsi inavyowatendea wafungwa katika gereza la Guantanamo yachomoza unapojaribu kutunga mfumo wa sheria ambao haulingani kabisa na misingi ya haki na sheria ziliokuwapo kabla.