Pigo kwa Poland na Bayern baada ya Lewandowski kupata jeraha
29 Machi 2021Timu ya taifa ya Poland imepata pigo baada ya mshambuliaji wake matata Robert Lewandowski kupata jeraha na hivyo basi kuikosa mechi ya kusaka tiketi ya kucheza michuano ya kombe la dunia nchini Qatar dhidi ya timu ya taifa ya England.
Kupitia taarifa, shirikisho la soka la Poland limesema mshambuliaji huyo ambaye pia ni anachezea klabu ya Bayern Munich amepata jeraha la goti na kwamba matibabu huenda yakachukua kati ya siku tano hadi kumi ili kupona.
Shirikisho hilo la soka limeandika katika tovuti yake, "Robert Lewandowski hatacheza mechi ya Jumatano dhidi ya England kutokana na jeraha."
Lewandowski alifunga mabao mawili katika mechi ya jana Jumapili dhidi ya Andorra na kufuatia jeraha hilo, atalazimika kurudi mjini Munich kwa uchunguzi zaidi wa kimatibabu na huenda akaikosa mechi ya Jumamosi dhidi ya RB Leipzig.
Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 32 amekuwa katika fomu nzuri msimu huu na tayari ameifungia Bayern Munich mabao 42 katika mashindano yote. Aidha alikuwa anaifukuzia rekodi ya ufungaji magoli ya Gerd Muller ya msimu wa 1971-1972 alipofunga mabao 40 kwa msimu mmoja.
Tayari Lewandowski alikuwa amecheka na nyavu mara 35 zikiwa zimesalia mechi nane pekee za Bundesliga. Jeraha lake bila shaka huenda likamuweka nje katika pambano muhimu dhidi ya mahasimu wao RB Leipzig Jumamosi ijayo 03.04.2021.