1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Pikipiki za bodaboda Uganda zatoa ajira na vurugu barabarani

23 Agosti 2024

Pikipiki za bei nafuu nchini Uganda zimekuwa baraka na laana kwa mji mkuu wa Kampala. Zinatoa ajira kwa sehemu kubwa ya vijana wa taifa hilo, lakini pia zinatazamwa kama kero ya mjini katika mitaa iliyosongamana.

Ruanda nach der Wahl 2024 | Straßenszene in Kigali
Picha: Luis Tato/AFP via Getty Images

Inaweza kuonekana kama mchezo wa kamari ya Urusi ya Roulette kwenye barabara za mji mkuu wa Uganda Kampala. Pikipiki hukatiza katikati ya magari, huvuka taa nyekundu na hubeba mizigo yenye ukubwa ambao hazikuundiwa kubeba.

Bodaboda zilipata jina lake kutokana na neno la Kingereza la border to border, ambalo lilikuwa neno maarufu la waendesha baiskeli waliokuwa wanauza bidhaa kati ya mpaka wa Uganda na Kenya.

Kwa waendesha bodaboda wa mjini Kampala, piki zao ni zana muhimu ya kujipatia kipato, iwe kwa kusafirisha bidhaa au abiria. Lakini kwa wengine, wakiwemo wauza maduka na watembea kwa miguu, boda boda ni kero ambayo wanatamani kuona ikidhibitiwa na kuwekewa miongozo.

Karibu nusu ya takribani boda boda 700,000 zinafanya kazi mjini Kampala, nyingi zikiandeshwa na wanaume wanaosema hakuna ajira nyingine kwao. Waendeshaji hao wanatokea sehemu zote za Uganda, na wameipa mitaa ya Kampala  muonekano wa vurugu kwa watazamaji.

"Tunafanya kazi hii kwa sababu hatuna kitu kingine cha kufanya, hatuna cha kufanya. Hata sisi sote hapa, watu wengine ni wahitimu wa shahada, wana shahada zao za uzamili, lakini wapo tu hapa hawana cha kufanya, ndugu yangu," anasema dereva bodaboda Zubairi Idi Nyakuni wakati akisubiri wateja mjini kati.

Soma pia: Shughuli za kiuchumi zaanza kurejea nchini Uganda

Madereva boda-boda hao, wanaofanya shughuli zao kwa sehemu kubwa bila udhibiti wa seriali, wamepinga juhudi za karibuni kuwaondoa kutoka kwenye mitaa miembamba ya kitovu cha biashara cha jiji la Kampala.

Shahada si kizuizi kufanya kazi ya bodaboda

02:36

This browser does not support the video element.

Hili linawafadhaisha wakuu wa jiji ambao wanataka kusafisha eneo hilo na wanasisitiza hofu ya serikali kuhusu matokeo ya kukasirisha kundi kubwa la wanaume hao wasio na kazi.

Je, serikali imeshindwa kuielewa sekta hiyo?

Charles Mwanguhya ni meneja wa masuala ya ushirika wa kampuni ya Stimme ambayo imekuwa ikifadhili maelfu ya vijana katika ndoto zao za kununua pikipiki, anasema serikali imeshindwa kuielewa sekta hiyo.

Karibu asilimia 76 ya wakaazi wa Uganda milioni 43 ni wenye umri wa chini ya miaka 35 kulingana na takwimu za serikali.

Ajira ni nadra na zile zinazolipa vizuri zaidi ni ngumu hata zaidi kupatikana katika uchumi ambako asilimia moja tu ya wafanyakazi milioni 22.8 wanaingiza dola 270 au zaidi katika mshahara wa mwezi, kwa mujibu wa takwimu za Benki Kuu zilizotolewa mapema mwaka huu wa 2024.

Kiwango cha ukosefu wa ajira nchini Uganda - kama sehemu ya watu wasio na ajira kwa jumla ya nguvu kazi - kiliongezeka kutoka asilimia tisa mwaka 2019 hadi asilimia 12 mwaka 2021, kulingana na utafiti wa hivi karibuni zaidi wa Ofisi ya Takwimu ya Uganda.

Kiwango cha ukosefu wa ajira kwa vijana kati ya umri wa miaka 18 na 30 kilikuwa kikubwa zaidi, kwa asilimia 17, na kwa vijana katika maeneo ya mijini kilikuwa asilimia 19.

"Tunapaswa kufahamu Boda Boda inakotokea na jinsi ilivyokua. Una watu, tumekuwa sensa ya makazi na watu ... hadi asilimia 72 ni vijana chini ya umri wa miaka 35, kwa hivyo una idadi kubwa ya watu ambao ni vijana, ambao hawawezi kupata kazi ya kufanya - iwe katika sekta ya umma au sekta binafsi na hawana kipato kikubwa mbadala kuweza kushiriki katika biashara nyingine. Hivyo pikipiki inakuwa kitu rahisi.

Soma pia: Msemaji mkuu wa Polisi Uganda auawa

Lakini jambo la pili,  hasa katika maeneo ya mijini ya Uganda ambayo huna usafiri wa umma, huna mabasi, huna treni, huna tramu, pikipiki inakuwa njia rahisi zaidi ya kuzunguka," anasema Charles Mwanguhya.

Pikipiki kama njia ya usafiri iliibuka kwenye mpaka wa Uganda na Kenya wakati wa kipindi cha machafuko ya kisiasa katika miaka ya 1970. Wakati huo, pikipiki ziligeuka njia ya haraka na rahisi ya kusafirisha walanguzi wa magendo na bidhaa zao katika ya miji ya mpakani.

Tanzania: Madereva wa bodaboda Mtwara waelimishwa kuhusu uendeshaji salama

02:39

This browser does not support the video element.

Na sasa, ikizidi kuenea katika kila mji wa Uganda tangu mwanzo wa karne, boda boda hutimiza majukumu mengi; kuanzia kuwapeleka watoto shule, kubeba mizigo, kutumika kama teski kuwapeleka watu ofisini kwao, na hata kuwasafirisha wafu kwenye majeneza.

Wanaume wengi wa boda-boda hununua pikipiki zao kwa mkopo kupitia makampuni kama vile virtue, lakini wengine wanafanya kazi kwa wafanyabiashara wanaonunua pikipiki kwa wingi na kuzisambaza miongoni mwa madereva wanaotakiwa kutuma malipo ya kawaida.

Polisi yalaumiwa kusababisha ajali

Lakini utamaduni wa kutofuata sheria za trafiki na usalama barabarani umekithiri miongoni mwa waendesha bodaboda.

Innocent Aweta, mwendesha boda-boda ambaye aliacha shule ya sekondari mwaka wa 2008, anasema kuna "shinikizo kubwa" la kuhifadhi pikipiki yake: anatakiwa kumlipa mwajiri wake kiwango sawa na dola 4 za Marekani kwa siku, mbali ya kuitunza pikipiki yake na kuitia mafuta.

"Kitu kinachosababisha ajali ni polisi, ukifika kwenye taa ya barabarani mtu anakuja tu na kukamata funguo yako ndiyo maana boda boda, tunapita tu, tunavunja sheria hiyo tu. Wakati mwingine wengine wanatumia njia moja ili uwe salama, pia huko uko salama ili uweze kuweka pesa yako, pesa ndogo uliyopata lakini wakikukamata, hiyo pesa ulioingiza, kama elfu 20 au 30, wanaichukua. Ndio maana watu wanaanza kuwatoroka polisi na kupita taa za trafiki na wakati mwingine barabara pia sio nzuri.

Soma pia: Kampala yageuka mji uliotelekezwa

Sheria za barabarani kwa ajili ya pikipiki, zilizoidhinishwa kwa mara ya kwanza mwaka 2004, ni ngumu kutekelezeka kwa sababu ya idadi kubwa ya boda-boda. Polisi wa usalama barabarani wanaweza tu kutazama wakati madereva boda-boda wakivuka taa za barabarani na kupita magari kwa njia ya hatari. Mara nyingi maafisa hao hawawezi kuwakamata kwa sababu ya kuhatarisha utaratibu wa umma.

Winstone Katushabe, Kamishna wa Usalama wa Usafiri kutoka Wizara ya Ujenzi na Usafiri anafafanua: "Tunahitaji kuwapa mafunzo, kuelewa namna wanavyotumia barabara, kuwa wavumilivu na watumiaji wengine wa barabara, kuhakikisha wako salama kwa sababu bado tunawahitaji, nimekuambia wengi wa vijana wana umri kati ya miaka 19 na 45, huu ndiyo umri wa uzalishaji zaidi kwa taifa lolote.

Ligi ya bodaboda

03:05

This browser does not support the video element.

Zana ya Museveni kuwadhoofisha wapinzani wake

Dhana ya boda-boda imekua kadiri Rais Yoweri Museveni alivyosalia madarakani. Katika miaka ya karibuni, akijaribu kudhoofisha uungaji mkono kwa wapinzani wake, Museveni amewazawadia boda-boda wafuasi wake na kuahidi kusababisha punguzo katika malipo ya leseni ya miaka mitano kutoka karibu dola 100 hadi karibu dola 27, chini ya sheria mpya zinazotazamiwa kutangazwa baadae mwaka huu, kwa mujibu wa bodi ya leseni za usafiri. Uamuzi huo utafanya iwe rahisi zaidi kwa Waganda kuwa wamiliki wa boda-boda.

"Tatizo letu si boda boda, tatizo ni udhibiti na kanuni zinazotumika kwa kila mtu kwa usawa pale ambapo una kundi fulani la watu wanaojaribu kuendesha juu ya sheria, wanaendesha upande usiyo sahihi wa barabara hawaheshimu sheria za barabarani, wanavunja sheria za trafiki utapata shida.

Soma pia: Burundi yapiga marufuku huduma za bodaboda mjini Bujumbura

Nitarejea kwa Tugende kwa mfano, tangu awali Tugende walianzisha utamaduni miongoni mwa madereva wao; moja lazima uwe umevaa kofia yako kila wakati, una vizibao vyako ambavyo serikali imekuwa ikijaribu kusisitiza sasa na kutekeleza, ikiwa utapita taa nyekundu na tukakukamata, huko nyuma ungetozwa faini kwa hilo. "Hivyo, tulikuwa na madereva wenye nidhamu barabarani," Mwanguhya anasema.

Bei ya boda-boda mpya ni karibu dola za Marekani 1,500. Kwenye mitaa iliyosongamana ya jiji la Kampala, boda-boda zinaonekana kama ishara ya uhuru na uwezo wa kujikimu kimaisha.

Chanzo: APTN

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW