Pistorius akana wito wakufanya mageuzi ya uongozi SPD
23 Machi 2026
Pistorius ameelezea kwamba kwa sasa hana nia ya kuongeza majukumu kwenye chama hicho.
Chama cha SPD, ambacho kimekuwa kikiongoza serikali za muungano katika jimbo la Rhineland-Palatinate kwa miaka 35 mfululizo, kiliondolewa katika nafasi hiyo ya juu na chama cha Christian Democrats (CDU) cha Kansela Friedrich Merz katika uchaguzi huo wa Jumapili.
Matokeo ya awali yanaonesha kwamba chama cha CDU kimeibuka mshindi kwa kupata asilimia 31, kikifuatiwa na SPD kilichojinyakulia asilimia 25.9 ya kura.
Matokeo hayo ndiyo mabaya zaidi kwa Wasoshalisti katika jimbo hilo ambalo katika uchaguzi uliopita wa mwaka 2021 kilipata asilimia 35.7. Chama cha siasa kali za mrengo wa kulia cha AfD kilijiongezea umaarufu kikishikilia nafasi ya tatu kwa kupata asilimia 19.5 ambayo ni matokeo yao mazuri ya kihistoria Magharibi mwa Ujerumani.
Akizungumza na shirika la habari la DPA wakati wa ziara yake mjini Tokyo, Pistorius ameyaelezea matokeo ya uchaguzi wa jimbo la Rhineland-Palatinate kuwa mabaya lakini amesisitiza kuwa sio sababu ya kuvunja sifa ya kampeni ya nguvu iliyofanywa na waziri mkuu wa jimbo hilo, Alexander Schweitzer.
Uchaguzi wa jimbo la Rhineland-Palatinate pigo kwa SPD
Waziri huyo wa ulinzi wa Ujerumani amesema kwa sasa chama hicho pamoja na muungano uliopo hauhitaji mijadala binafsi kuhusu masuala ya uongozi, na kwamba katika muda huu hawezi kupatikana kwa mijadala kama hiyo.
"Kutokana na yanayoendelea kwa sasa duniani na changamoto tunazopitia nchini Ujerumani, tuna matatizo mengi ya kushughulikia na lazima tujikite katika kazi zetu serikalini," alisema Boris Pistorius.
Pistorius, ambaye mara nyingi amekuwa akionekana kama mwanasiasa maarufu wa chama cha SPD na mashuhuri kabisa katika siasa za Ujerumani, amesisitiza kwamba kinachopaswa kuzingatiwa kwa wakati huu ni kazi ya serikali na sio mabadiliko binafsi ya uongozi.
Kauli yake ameitoa baada ya mbunge wa SPD Doris Schröder-Köpf kutaka kufanyike mabadiliko makubwa ya uongozi na kumpendekeza Waziri Mkuu wa Saarland, Anke Rehlinger na Pistorius wachukue nafasi za juu, ikiwemo kumrithi Naibu Kansela ambaye pia ni waziri wa Fedha Lars Klingbeil.
Uchaguzi wa Jumapili ulikuwa pigo kwa chama cha SPD ambacho ni kikongwe zaidi katika siasa za nchini Ujerumani. Chama cha kijani pia kilimshinda mgombea wa Social Democrats aliyekuwa madarakani kwa muda mrefu, Dieter Reiter, katika uchaguzi wa meya wa Munich ambao ni mji mkuu wa jimbo la Bavaria.