Poland haitasaini mkataba wa Lisbon
1 Julai 2008Hatua ya rais Lech Kacynski kusema hatosaini mkataba wa Lisbon kwa sasa ni pigo lengine kubwa kwa Umoja wa Ulaya katika juhudi zake za kutaka mkataba huo uidhinishwe na nchi wanachama. Kiongozi huyo amesema haina maana kuuidhinisha mkataba huo baada ya wananchi wa jamhuri ya Ireland kuukataa katika kura ya maoni iliyofanyika Juni 12.
Rais Kacynski alisaidia katika matayarisho ya mkataba huo lakini sasa chama chake kinaupinga. Kiongozi huyo wa Poland amesema ni vigumu kusema swala hili litamaliza vipi lakini si sahihi kusemakwa kuwa hakuna mkataba hakuna muungano. Ameonya kwamba jamhuri ya Ireland haitakiwi kulazimishwa kupitisha uamuzi usio wake.
Waziri mkuu wa Poland, Donald Tusk amemkosoa vikali rais Kaczynski na kusema hiyo si njia nzuri ya kujenga sifa ya Poland katika ngazi ya kimataifa. Spika wa bunge la Poland, Bronislaw Komorowski, pia amemkosoa rais Kaczynski.
´Matamshi ya rais yananitia wasiwasi kwa sababu Poland inatakiwa kuwa sehemu ya nchi za Umoja wa Ulaya. Kuisaidia jamhuri ya Ireland kuutanzua mzozo wake na wakati huo huo Poland yenyewe iuidhinishe mkataba wa mageuzi wa Umoja wa Ulaya haraka iwezekanavyo. Bunge la Poland limekamilisha kazi yake na sasa rais analazimika kusaini mkataba huo ambao yeye mwenye alihusika katika mazungumzo ya kuutayarisha.´
Marek Safjan, jaji mkuu wa mahakama ya katiba nchini Poland ana wasiwasi kuhusu matamshi ya rais Kacynski na amesema hayaendani na katiba.
´Kwa wasiwasi mkubwa ninaona tunaweza kutumbukia katika matatizo makubwa iwapo tutatilia shaka kuidhinishwa kwa mkataba huu. Ninarudia tena masimamo wangu kwamba baada ya bunge kukubaliana kuuidhinisha mkataba, rais hatakiwi tena kukataa. Anatakiwa ikiwa ana haki kikatiba kutilia shaka uamuzi wa bunge, basi awasilishe wasiwasi wake kwa mahakama ya katiba. Kwa kuwa hilo halifanyi, anatakiwa asaini mkataba huo haraka.´
Msimamo wa rais Kacynski ni pigo kubwa kwa rais wa Ufaransa Nicholas Sarkozy ambaye anataka kutafuta njia ya kuubadili uamuzi wa Ireland kuhusu mkataba wa Lisbon katika miezi sita ambapo Ufaransa itashikilia urais wa Umoja wa Ulaya. Ufaransa leo imesema inataka kufanya mazungumzo na viongozi wa Poland kuhusu mkataba huo.
Kiongozi wa ofisi ya rais Slawomir Novak amesema matamshi ya rais Kaczynskiya aina hiyo hayausaidii tena Umoja wa Ulaya wakati huu mgumu. Kiongozi huyo ameongeza kusema litakuwa jambo baya ikiwa wananchi wa Poland wataanza kuyazungumzia matamshi ya rais wao nchini kote.
Wakati huo huo rais wa Ujerumani Horst Kohler hatakamilisha mchakato wa kuuidhinisha mkataba wa Lisbon mpaka mahakama kuu ya katiba itakapopitisha uamuzi kuhusu mashitaka yaliyowasilihwa kuzuia kuidhinishwa kwa mkataba huo na Ujerumani.