1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Poland ijitoe?

21 Juni 2007

Leo hii umeanza mkutano wa kilele wa viongozi 27 wa nchi za Umoja wa Ulaya. Mazungumzo yao yanatarajiwa kuwa magumu kwani kuna suala moja ambalo limezusha mvutano kati ya nchi wanachama: Poland ambayo imejiunga hivi karibuni tu na Umojo huo, haitaki kukubali mkataba mpya ikipinga hasa namna ya kupiga kura.

Kwa mujibu wa Poland, nchi kubwa kama Ujerumani yenye raia wengi itapewa uzito mno katika mfumo huu uliopendekezwa. Huu kwanza ni uchambuzi wa gazeti la “Berliner Morgenpost”:

“Kusema ukweli, Poland ina sababu nzuri za kupinga mfumo wa kupiga kura. Tena haiko peke yake, kwani ni mwanadiplomasia wa Sweden ambaye alikuwa wa kwanza kuukosoa mfumo huo mpya unaozingatia idadi ya wananchi. Nchi kadhaa ndogo wanachama wa Umoja wa Ulaya wana wasiwasi juu ya mfumo wa kupiga kura ambao unazinufaisha nchi kubwa. Hata hivyo lakini, viongozi wa Poland, ndugu wawili, , hakuna wanaojitokeza kuwaunga mkono, kwa sababu nia zao za kweli hazijulikani.”

Mhariri wa “Nürnberger Nachrichten” anataja wasiwasi wake juu ya mustakabali wa Umoja wa Ulaya. Ameandika:

“Sera hizo za Poland za za kupinga mfumo wa kupiga kuwa zisiruhusiwe kuuzuia kabisa Umoja wa Ulaya katika kufanya kazi. Umoja huu hauwezi kusubiri hadi ndugu hao wawili watahapoondoshwa madarakani na wapiga kura wa Poland. Hata ikiwa Kansela Angela Merkel wa Ujerumani hataki Umoja wa Ulaya ugawanyike katika sehemu mbili, yaani moja ikiendelea haraka kushirikiana, na nyingine ikifuata taratibu, huenda hatakuwa na chaguo jingine ila tu kukubali pendekezo hilo lililotolewa na Italy la kuwepo na sehemu hizo mbili za Umoja huo. Hakuna njia nyingine, kwa sababu kulingana na mikataba ya Umoja wa Ulaya haiwezekani kuitenganisha nchi moja mwanachama kwa muda.”

Gazeti la “Landeszeitung” la mjini Lüneburg lakini lina pendekezo lingine la kutatua mzozo huu. Tunasoma:

“Bila shaka, kila nchi wanachama ina haki ya kupigania maslahi yake na kuwa na msimamo wake, hata kutumia maneno makali ikiwa yanahitajika. Kimsingi basi, Poland inatumia haki yake tu. Lakini kutokubaliana kutaweza kuiathiri Poland ambayo ni nchi inayopata sehemu kubwa kabisa ya msaada kutoka kwa Umoja wa Ulaya. Kwani Umoja huu ambao hautakubali kulazimishwa, hatimaye utabakia na njia moja, tu, yaani kutoa kadi nyekundu na kuwaambia viongozi wa Poland: Basi, ikiwa hamutaki kukubali sheria za mchezo, mnapaswa kutoka uwanjani.”

Ni gazeti la “Landeszeitung”. Na hatimaye tunamnukuu mhariri wa “Wiesbadener Kurier” ambaye pia anataka uamuzi ambao hautaathiri Umoja wa Ulaya:

“Si kama Umoja wa Ulaya bado ni mtoto mchanga au ni kama ushirikiano ambao umeanza tu kuridhiana, bali sasa unataka kufaulu katika mtihani huu wa kumaliza shule. Haitawezekani kuuandika upya na upya hadi wanachama wote wameridhika kabisa. Ili kuchukua maamuzi ya msingi, itabidi kujipa moyo na kutouzuia ushirikiano huu katika maendeleo yake ili njia iwe wazi. Hata ikiwa itabidi kujitoa.”