1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Poland: Kombora huenda lilirushwa kutoka Ukraine

16 Novemba 2022

Rais wa Poland Andrzej Duda amesema hakuna ishara kwamba kombora lililoangukia nchini humo na kuwaua watu wawili, lilikuwa shambulizi la kukusudia katika nchi ya Jumuia ya Kujihami ya NATO.

Explosion in Polen nahe Grenze zur Ukraine
Picha: Pawel Supernak/PAP/dpa/picture alliance

Duda amesema inawezekana jeshi la anga la nchi jirani ya Ukraine ndilo lilirusha kombora hilo la enzi ya utawala wa Kisovieti. Akizungumza Jumatano na waandishi habari, Duda amesema kuwa jeshi la Ukraine lilikuwa likirusha makombora yake kuelekea kwenye maeneo mbalimbali na kwamba bahati mbaya kombora moja likaangukia kwenye ardhi ya Poland. ''Hakuna ishara inayoonesha kwamba shambulizi hili lilikuwa linailenga Poland.

Uwezekano mkubwa zaidi lilikuwa shambulizi la bahati mbaya. Urusi jana iliishambulia Ukraine. Mifumo ya kujilinda na makombora ya Ukraine pia ilirushwa ili kujikinga na shambulizi la Urusi. Na hakuna ushahidi kwamba kombora hilo lilirushwa na Urusi,'' alifafanua Duda.

NATO iko katika hali ya tahadhari

Shambulizi hilo limeiweka NATO katika hali ya tahadhari. Mabalozi wa NATO wanakutana kwa kikao cha dharura leo kuzungumzia shambulizi hilo. Hata hivyo, Rais wa Marekani Joe Biden amewaambia viongozi wenzake wa kundi la nchi zilizoendelea na zinazoinukia kiviwanda za G20 kwamba dalili zinaonesha kwamba kombora hilo la kuzuia mashambulizi limerushwa kutoka Ukraine, huku Waziri Mkuu wa Uingereza, Rishi Sunak akiilaumu Urusi kwa kufanya mashambulizi hayo kuwa muhimu.

Katibu Mkuu wa NATO, Jens Stoltenberg amesema kuwa shambulizi hilo la Poland huenda limerushwa na Ukraine, lakini Urusi inabeba dhamana ya mwishio katika vita hivyo. Akizungumza mjini Brussels, baada ya kuendesha kikao cha mabalozi wa NATO, Stoltenberg amesema uchunguzi wa tukio hilo unaendelea, na wanahitaji kusubiri matokeo yake. Amesema uchunguzi wa awali unaonesha Ukraine ilirusha kombora hilo kwa ajili ya kujilinda na mashambulizi ya makombora yanayofanywa na Urusi.

Katibu Mkuu wa NATO, Jens StoltenbergPicha: Valeria Mongelli/ZUMA Press Wire/dpa/picture alliance

Kwa upande wake Urusi imeishutumu Ukraine kwa shambulizi hilo la Poland, huku Waziri wa Mambo ya Nje wa Ubelgiji Ludivine Dedonder, akisema huenda Ukraine ilirusha kombora hilo kujikinga na mashambulizi kutoka Urusi. Wizara ya ulinzi ya Urusi imesema picha za mabaki ya kombora hilo zilitambuliwa na wataalamu wa jeshi la Urusi kama vipande vya mfumo wa kujilinda kombora la Ukraine chapa S-300 la mfumo wa anga wa kujikinga na makombora. Aidha, Ikulu ya Urusi, Kremlin imeipongeza Marekani kwa namna ilivyotoa msimamo wake kuhusu shambulizi hilo.

Ukraine imesema inataka kuruhusiwa kwenda kwenye eneo ambako shambulizi limetokea. Afisa wa ngazi ya juu wa ulinzi wa Ukraine, Oleg Danilog amesema nchi hiyo ina ushahidi kwamba ''Urusi inahusika'' katika shambulizi hilo, bila ya kutoa taarifa zaidi.

Macron: Marekani ilitoa taarifa za awali

Wakati huo huo, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amesema Marekani ilitoa taarifa za awali kuhusu shambulizi la Poland, lakini ilikuwa ni mapema mno kusema kile kilichotokea. Akizungumza Jumatano na waandishi habari huko Bali, Indonesia baada ya mkutano wa kilele wa G20, Macron amesema wanapaswa kuwa makini.

Msemaji wa serikali ya Ujerumani amesema kuanzisha eneo la kutoruhusu ndege kuruka kutasababisha kitisho cha makabiliano ya moja kwa moja kati ya Urusi na NATO. Amesema Ujerumani pamoja na washirika wao wamekubaliana kwamba wanataka kuzuia mivutano zaidi ya vita vya Ukraine. Aidha, Ujerumani pia itatoa msaada wa kijeshi kwa Poland

Huku hayo yakijiri, viongozi wa G20 wamekamilisha mkutano wao nchini Indonesia kwa kutoa tamko la kulaani vita vya Ukraine na kuonya kuwa mzozo huo unaufanya uchumi wa dunia ambao tayari umedorora kuwa mbaya zaidi.

(AFP, AP, DPA, Reuters)

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW