1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Poland kuonyesha uthabiti wake inapoongoza Umoja wa Ulaya

Bakari Ubena Jacek Lepiarz
4 Januari 2025

Poland inayoshikilia uenyekiti wa kupokezana wa Umoja wa Ulaya, imedhamiria kuonyesha uongozi thabiti hasa katika sekta za ulinzi na usalama.

Bendera ya Poland (kulia) na ile ya Umoja wa Ulaya
Bendera ya Poland (kulia) na ile ya Umoja wa UlayaPicha: Beata Zawrzel/IMAGO

Kuanzia Januari 1, 2025, Hungary iliikabidhi Poland kijiti cha urais wa kupokezana wa Umoja wa Ulaya, na hivyo kuhitimisha miezi sita ya msukosuko ndani ya umoja huo. Hayo ni wakati mataifa mawili yenye uchumi mkubwa barani Ulaya ya Ujerumani na Ufaransa yakikabiliwa na migogoro ya kisiasa. 

Badala ya kuwa mpatanishi asiyeegemea upande wowote, Waziri Mkuu wa Hungary Viktor Orban alisababisha msuguano na  taasisi za EU mjini Brussels  na kuwakasirisha washirika wake baada ya kuanzisha kile alichokiita "ujumbe wa amani" na kufanya ziara za kushtukiza huko Moscow, Kyiv na Beijing, ziara ambazo hazikuamuliwa na nchi wanachama.

Kai-Olaf Lang, mtaalamu wa masuala ya Ulaya Mashariki katika Taasisi ya Ujerumani inayofuatilia siasa za Kimataifa na Usalama anatabiri kuwa urais wa Poland wa kuongoza Baraza la Umoja wa Ulaya, utakuwa kinyume na kile kilichotokea katika kipindi cha miezi sita iliyopita chini ya uongozi wa Hungary. Lang ameiambia DW kwamba tofauti hiyo itadhihirika hasa katika sera ya usalama ya Umoja wa Ulaya pamoja na uhusiano na Ukraine na Urusi.

Tusk: "Mwanasiasa mzoefu"

Waziri Mkuu wa Poland Donald TuskPicha: Antoni Byszewski/Fotonews/Newspix/IMAGO

Waziri Mkuu wa Poland Donald Tusk ni mwanasiasa mzoefu barani Ulaya. Alikuwa rais wa Baraza la Ulaya kuanzia mwaka 2014 hadi 2019 na baadaye akawa mwenyekiti wa Chama cha Watu wa Ulaya (EPP) chenye viti vingi katika Bunge la Ulaya.

Baada ya miaka minane ya serikali iliyokuwa ikioongozwa na chama cha kihafidhina cha Sheria na Haki (PiS), muungano wa Tusk ulishinda uchaguzi mkuu nchini Poland zaidi ya mwaka mmoja uliopita.

Katika hotuba yake ya kwanza baada ya kushika wadhifa wa waziri mkuu wa Poland mwezi Desemba 2023, Tusk alitangaza kwa ujasiri kwamba "hakuna anayeweza kumshinda ndani ya Umoja wa Ulaya."

Poland kudhihirisha uzoefu wake

Waziri Mkuu wa Poland Donald Tusk (kulia) akiwa na rais wa Ufaransa Emmanuel MacronPicha: Monika Sieradzka/DW

Urais wa kupokezana wa Baraza la  Umoja wa Ulaya (EU) ni fursa mwafaka kwa Donald Tusk kuonyesha kwamba mapambano yake ni zaidi ya kauli na kwamba miaka 20 baada ya Poland kujiunga na EU, nchi hiyo si changa tena kwenye masuala ya uongozi lakini inaweza hata kuzionyesha baadhi ya nchi kubwa wanachama namna ya kushughulikia mambo kadhaa.

Adam Szlapka, Waziri wa Poland anayehusika na masuala ya EU, alisema hivi karibuni wakati akiwasilisha vipaumbele vya Poland wakati wa urais wa Baraza la EU kwamba nchi yake inaaminika na sera zake zinakubalika, huku akiongeza kuwa nchi hiyo imekuwa "mtaalamu wa changamoto kubwa" zinazoyakabili mataifa ya Magharibi.

Hoja muhimu kuhusu masuala ya usalama

Kwa miezi kadhaa sasa, hotuba za Tusk zimekuwa zikitoa wito wa kuifanya sera ya usalama wa Poland na nchi nyingine zilizopo kwenye eneo la mashariki mwa wanachama wa NATO, kuwa sera ya pamoja ya Umoja wa Ulaya.

Soma pia: Poland yatoa msaada wa makombora kwa Ukraine

Mwishoni mwa mwezi Novemba, Tusk alisema kabla ya mkutano wa kilele wa NB8 wa nchi nane za Nordic na Baltic huko nchini Sweden kwamba Ulaya inapaswa kuimarisha uhusiano wake na Marekani, lakini ni lazima iwe huru na iweze kusimama yenyewe. Tusk alisisitiza kuwa wakati ni sasa wa kumaliza "enzi ya kutokuwa na uhakika na kuwa na hofu kwa ajili ya Urusi."

Askari wa Poland akishika doriaPicha: Kamil Jasinski/NurPhoto/picture alliance

Ili kuwa tayari kwa lolote linaloweza kutokea, Poland inaunda safu ya ulinzi eneo la mashariki mwa Ulaya inayoitwa "East Shield" kwenye mpaka wake na Belarus na ingependa Umoja wa Ulaya usaidie kuufadhili mpango huo. Serikali mjini Warsaw pia inashiriki katika mpango wa ulinzi wa anga wa Ulaya unaojulikana kama European Sky Shield.

Pia, Waziri huyo Mkuu wa Poland amedhamiria kuzuia uwezekano wa mazungumzo yoyote kukomesha vita nchini Ukraine  ambayo yatautenga Umoja wa Ulaya na ambayo yanaweza kuanza katika msimu huu wa baridi.

Poland ambayo imo katika hali ya kampeni za uchaguzi wa kumsaka rais mpya anayetakiwa kuchaguliwa mwezi Mei mwakani, inashinikiza pia kuanza kwa mazungumzo kuhusu kuanzisha mchakato wa Ukraine kujiunga na Umoja wa Ulaya.

(DW)

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW