Poland yaishutumu Urusi kwa kupanga 'ugaidi wa angani'
15 Januari 2025Akizungumza mjini Warsaw baada ya mkutano wake na Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, Tusk amesema vifurushi vilivyolipuka katika bohari za vifaa kwenye nchi kadhaa za Ulaya zilikuwa sehemu ya jaribio la Urusi la njama ya kusababisha milipuko kwenye ndege za mizigo kwenda Marekani.
Soma pia;Poland kuonyesha uthabiti wake inapoongoza Umoja wa Ulaya
Milipuko hiyo ilitokea katika bohari huko Uingereza, Ujerumani na Poland mwezi Julai. Hata hivyo, Urusi imekanusha kuhusika.
Tusk amesema, "Taarifa za hivi punde zinaweza kuthibitisha uhalali wa hofu kwamba Urusi inapanga vitendo vya ugaidi wa angani - sio tu dhidi ya Poland, bali pia dhidi ya mashirika ya ndege duniani kote."
Poland, ambayo kwa sasa inashikilia urais wa zamu wa miezi sita katika Umoja wa Ulaya, na mwanachama wa Jumuia ya Kujihami ya NATO imekuwa moja ya washirika wakubwa wa Ukraine tangu Urusi ilipoanzisha vita dhidi ya Kyiv mnamo Februari 2022. Tusk ameahidi kutumia nafasi ya nchi yake kama mwenyekiti wa zamu Umoja wa Ulaya, kutilia mkazo ombi la Ukraine la kutaka uwanachama katika jumuiya hiyo.
Soma pia: Tusk atarajia kutatuwa mgogoro wa Poland na Ukraine
Zelesky asisitiza zaidi kujiunga na Umoja Ulaya
Zelensky aliwaambia waandishi wa habari kwamba mara tu Ukraine itavyojiunga katika Umoja wa Ulaya, ndivyo Ukraine itakavyokuwa mwanachama wa NATO, ndivyo watakuwa na ushirikiano zaidi, na Ulaya nzima ndivyo itakavyopata uhakika wa kisiasa wa kijiografia inayohitaji.
Akizungumzia usalama wa Ukraine, Zelensky amesema kwamba kupelekwa kwa wanajeshi wa kigeni nchini Ukraine ni hatua inayoweza tu kuwa sehemu ya hakikisho la kiusalama, lakini haiwezi kutosheleza usalama wa taifa hilo.
"Baada ya siku 5, Rais Trump ataapishwa nchini Marekani. Tunatarajia ushirikiano wa dhati katika muelekeo wa amani."
"Tunategemea kuimarishwa kwa vikwazo dhidi ya Urusi kwa kupigana vita - sauti ya Poland ni muhimu katika suala hili. Awamu ya 16 cha vikwazo kinatayarishwa na Umoja wa Ulaya." Alisema Zelensky.
Soma pia: Tusk aahidi kuendelea kuisaidia Ukraine
Zelensky ameitembelea Poland baada ya nchi hizo mbili kufikia makubaliano kuhusu mvutano wa miongo kadhaa juu ya mauaji ya Wapoland yaliyofanywa na wazalendo wa Ukraine, wakati wa Vita vya Pili vya Dunia.
Urusi na Ukraine wabadilisha wafungwa
Tukiangalia yanayojiri nyanjani nchini Ukraine na Urusi, maelfu ya wapiganaji wamerudishwa katika makubaliano ya kubadilishana wafungwa mara kadhaa tangu Urusi ilipoivamia Ukraine mnamo Februari 2022, ushirikiano ambao ni nadra kati ya Moscow na Kyiv baada ya mapigano ya karibu miaka mitatu.
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesema watu 25 wanarudi nyumbani Ukraine, ikiwa ni pamoja na baadhi ya waliopigana katika kiwanda cha chuma cha Azovstal kwenye mji wa kusini wa Mariupol, uliotekwa na Urusi mnamo Mei 2022.
Urusi kwa upande wake imesema wanajeshi wake wameanza kupewa msaada muhimu wa kisaikolojia na matibabu huko Belarus, kabla ya kurejea Urusi.