1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Poland yaonya kuhusu wimbi kubwa la wakimbizi kuelekea Ulaya

18 Novemba 2021

Waziri mkuu Mateusz Morawiecki asema nchi yake iko tayari kuilinda kwa hali yoyote mipaka yake ikiwa Belarus itazidisha uchokozi kuelekea Poland

Polen Grenze zu Belarus | Migranten
Picha: Barbara Wesel/DW

Waziri mkuu wa Poland  Mateusz Morawiecki ametowa tahadhari kwamba Ulaya itapokea wimbi la mamilioni ya wahamiaji ikiwa sera kuhusu mipaka hazitoimarishwa.Tamko la kiongozi huyo wa Poland limekuja wakati bado maelfu ya wahamiaji wakiendelea kujaribu kuingia ulaya.Lakini pia mashirika ya ndege sasa yamekubali kuwazuia kusafiri watu ambao huenda wanataka kwenda Belarus kutafuta hifadhi.

Waziri mkuu wa Poland Mateusz Morawiecki alikuwa akizungumza na gazeti la Ujerumani la Bild na katika mahojiano hayo ndipo aliposema kwamba  ikiwa Umoja wa Ulaya utashindwa kuwazuia maelfu ya wahamiaji hivi sasa kuingia basi hivi karibuni mamia kwa maelfu na mamilioni watafunga safari kuelekea barani Uaya.

Picha: Barbara Wesel/DW

Kufuatia hali ya sasa katika mpaka baina ya nchi yake la Belarus waziri mkuu huyo wa Poland hakuondowa uwezekano wa kutokea vita. Morawiecki ameendelea kusema kwamba ikiwa Ulaya haitoamua kulinda na kutetea mipaka yake mamilioni ya wahamiaji kutoka Afrika na Mashariki ya kati watajaribu kuingia Ulaya na hasahasa nchini Ujerumani.

Lakini pia ameweka wazi kwamba kwa sasa hali katika mpaka wa nchi yake na Belarus  imedhibitiwa lakini kuna hatari inayoongezeka.Amelalamika kwamba vikosi vya Belarus vinaendelea na uchokozi zaidi na wa moja kwa moja ingawa amesema anataraji uchokozi huo hautopindukia mipaka kwasababu Poland iko tayari kutetea mpaka wake kwa namna yoyote.

Kingine alichokiweka wazi kwenye mahojiano hayo ni kwamba mpaka sasa hawafahamu Belarus na Urusi wanapanga kitu gani,akiongeza kusema kwamba inawezekana rais Vladmir Putin wa Urusi  anatumia mzozo huu kuwazubaisha watu ili kupanga  mashambulizi ya kijeshi dhidi ya Ukraine. Wakati huohuo vikosi vya Poland vimewakamata wahamiaji 100 waliokuwa wakijaribu kuvuka mpaka kutoka Belarus usiku wa kuamkia leo kwa mujibu wa wizara ya ulinzi ya nchi hiyo.

Na katika hatua nyingine kufuatia shinikizo kutoka Umoja wa Ulaya mashirika chungunzima ya ndege yamekubali kutowasafirisha wanaotaka kwenda kutafuta hifadhi ya ukimbizi Belarus.Aidha Iraq imesema itaanzisha mpango wa kuwarudisha kwa khiyari raia wake kutoka Belarus wiki hii. Shirika la ulinzi wa mipaka ya Umoja wa Ulaya Frontex nalo linashirikiana na Poland na mamlaka za Iraq kuandaa ndege za kuwasafirisha Wairaq kutoka Poland.

Lebanon nayo ni miongoni mwa nchi zilizoyaagiza mashirika yake ya ndege kuzuia wasafiri wanaokwenda Belarus,isipokuwa wale wenye Visa au vibali vya ukaazi wa kudumu wa nchi hiyo au wenye uraia.