1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Shambulizi la Urusi laua watatu huko Kharkiv, Ukraine

20 Machi 2024

Urusi imefanya mashambulizi katika mji wa kaskazini wa Kharkiv nchini Ukraine ambako watu watatu wameuawa na wengine watano wamejeruhiwa, huu ukiwa ni muendelezo wa mashambulizi yanaendelea baina ya nchi hizo mbili

Ukraine, Charkiw | Russischer Drohnen-Angriff
Mji wa Kharkiv nchini Ukraine umekuwa ukilengwa zaidi katika mashambulizi yanayofanywa na Urusi nchini UkrainePicha: Sofiia Gatilova/REUTERS

Urusi imefanya mashambulizi katika Mji wa kaskazini wa Kharkiv nchini Ukraine ambako watu watatu wameuawa na wengine watano wamejeruhiwa, huu ni muendelezo wa mashambulizi ya pande zote mbili ambayo yanaendelea katika maeneo ya mipaka ya nchi hizo. Wakati mashambulizi hayo yakijiri, Poland imepeleka msaada wa makombora ya Taurus nchini Ukraine huku ikiilaumu Ujerumani kwa kusita sita kupeleka Ukraine msaada wa vifaa vya kisasa vya kijeshi.

Soma zaidi. Borrell kupendekeza Umoja wa Ulaya kutumia mapato ya mali za Urusi zilizozuiliwa

Mji wa Kharkiv uliopo upande wa kaskazini nchini Ukraine na ambao unapakana na Urusi umekuwa ukishambuliwa mara nyingi zaidi tangu uvamizi wa Urusi kwa takribani miaka  miwili iliyopita.

Kupitia mtandao wa kijamii wa Facebook, Mkuu wa kitengo cha usalama katika mji huo Serhiy Bolvinov amesema Urusi imefanya shambulizi liliharibu nyumba ya uchapishaji na kiwanda cha rangi katika mji huo.

Shambulio la Urusi katika mji wa Kharkiv leo limeuwaua watu watatu na kuharibu nyumba na kiwanda cha rangi Picha: Vitalii Hnidyi/REUTERS

Shambulio hilo lilizusha moto mkali katika eneo la zaidi ya mita 1,000 za mraba, watu watatu wakipoteza maisha na wengine watano kujeruhiwa huku ikielezwa kwamba idadi yao inaweza kuongezaka.

Poland yatoa msaada wa makombora kwa Ukraine

Hata hivyo, wakati mashambulizi hayo yakiendelea katika maeneo hayo ya mipakani, Poland imetoa msaada wa makombora ya masafa marefu ya Taurus kwa Ukraine ili kuendelea kupambana na uvamizi wa Urusi.

Soma zaidi. Wakaazi wa maeneo ya mipakani ya Urusi na Ukraine watakiwa kuhama

Akizungumza na Shirika la habari la Dpa, Waziri wa mambo ya nje wa Poland Radoslaw Sikorski amesema msaada huo ni kwa lengo la Ukraine kujilinda yenyewe huku akiikosoa Ujerumani kwa mchakato mrefu wa kufanya maamuzi ya kutoa msaada wa vifaa vya kisasa  vya kijeshi kwa Ukraine.

Urusi yaukemea Umoja wa Ulaya

Hayo yakiendelea, Upande mwingine Urusi imekemea pendekezo la Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Josep Borrellla kutumia mapato ya mali zake zilizozuiwa kuisaidia Ukraine.

Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Josep Borrell amependekeza kutumia mapato yatokanayo na mali za Urusi zilizozuiwa barani Ulaya kuisaidia UkrainePicha: Virginia Mayo/AP/dpa/picture alliance

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa Urusi, Maria Zakharova amesema hii leo kuwa mapendekezo hayo ya Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Josep Borrell ya kutumia mapato yatokanayo na mali za Urusi zilizozuiwa barani Ulaya kuisaidia Ukraine, ni ujambazi na wizi. 

Soma zaidi. Urusi imehamisha watu elfu tisa kutoka mji wa Belgorod

Hii leo, Ukraine imepokea kifurushi cha kwanza cha msaada wa euro bilioni 4.5 kutoka kwa Umoja wa Ulaya. Hayo yanajiri wakati mapigano makali yameendelea kuripotiwa kati ya Moscow na Kyiv. Urusi imesema ilidungua droni 419 za Ukraine wakati wa uchaguzi huku hali ikizidi kuwa mbala katika eneo la mpakani la Belgorod.

Kwa upande wake , Waziri wa  Mambo ya Nje wa Ukraine, Dmytro Kuleba, ataizuru India wiki ijayo kujadili mpango wa amani na hii ikiwa ni ziara ya kwanza kwa kiongozi wa Ukraine tangu uvamizi wa Urusi miaka miwili iliyopita.

Ziara ya Kuleba inakuja kufuatia mwaliko wa serikali ya India ikiwa ni baada ya Rais wa India Narendra Modi kumpigia simu Rais wa Ukraine Volodymyry  mapema mwaka huu.