Polisi 3 wakamatwa Kenya kwa kumburuta mwanamke ardhini
11 Juni 2020Kwenye video iliyorekodiwa kwa muda wa dakika moja na nusu mnamo siku ya Jumatano eneo la Kuresoi Kusini, magharibi ya mji mkuu wa Nairobi, afisa wa polisi anaonekana akiendesha pikipiki huku akimburuta mwanamke aliyefungwa kwenye pikipiki hiyo akiwa chini barabarani, huku maafisa wengine wakimchapa.
Kisa hicho kilifanya suruali ndefu aliyoivaa wakati huo kumtoka na hivyo kumuacha nusu uchi.
Kulingana na mamlaka ya umma inayochunguza malalamiko dhidi ya utendakazi wa polisi nchini Kenya (IPOA), mwanamke huyo alituhumiwa kuingia katika nyumba ya afisa wa polisi akijaribu kuiba.
Idara ya uchunguzi wa makosa ya jinai nchini Kenya imesema kupitia taarifa kuwa maafisa watatu wametiwa nguvuni, baada ya kanda hiyo ya video kusambaa mitandaoni, na kwamba washukiwa hao wanashikiliwa wakati uchunguzi wa kisa hicho ukiendelea.
Chunguzi dhidi ya kisa hicho zaendelea
Mamlaka ya IPOA pia imesema kuwa imeanzisha uchunguzi kuhusiana na kisa hicho.
Maafisa hao wamekamatwa mnamo wakati kuna ghadhabu nyingi nchini Kenya kutokana na visa vya polisi kutumiaji nguvu kupita kiasi dhidi ya watuhumiwa.
Aidha kukamatwa kwa maafisa hao kumejiri mnamo wakati kifo cha Mmarekani mweusi Geotrge Floyd nchini Marekani ambacho pia kilitokana na ukatili wa polisi, kimechochea maandamano makubwa ulimwenguni na hata barani Afrika ambako mara kwa mara polisi huwashambulia watuhumiwa bila kuzingatia haki.
Mnamo Jumatatu, takriban watu 200 waliandamana mjini Nairobi wakilaani vifo vya watu 15 mikononi mwa polisi tangu amri ya kutotoka nje usiku ilipotangazwa mwezi Machi ili kupambana na usambaaji w avirusi vya corona.
Shutuma dhidi ya polisi nchini Kenya
Vikosi vya polisi nchini Kenya mara kwa mara hushtumiwa na makundi ya kutetea haki za binadamu kwa kutumia nguvu kupita kiasi na kuwaua watu kiholela, hasa katika mitaa ya watu maskini.
Wiki iliyopita, mchambuzi na pia mchoraji vibonzo kutoka Kenya Patrick Gathara alichora katuni ikionyesha serikali za Afrika zikiwa zimeyabeba mabango yenye ujumbe "BlackLivesMatter yaani uhai wa watu weusi ni muhimu, huku wakimkandamiza mtu shingoni akilia na kuuliza je Uhai wa Waafrika pia ni muhimu?
Kwenye ujumbe wake kwa njia ya maoni yaliyochapishwa kwenye gazeti la Afrika Kusini 'South Africa's Mail' na pia The Guardian, Somolon Dersso ambaye ni mwenyekiti wa Tume ya haki za binadamu ya Afrika alilihimiza bara la Afrika kuwa na mjadala unaohitajika sana kuhusu mauaji hayo pamoja na visa vya ukatili kutoka kwa maafisa wa polisi, hasa katika kipindi hiki cha janga la corona. Ameongeza kuwa kuwa mjadala huo unapaswa kuambatana na ghadhabu tele.
Mauaji ya George Floyd, hayajasababisha maandamano makubwa barani Afrika lakini mara kwa mara wanaharakati barani Afrika wamekuwa wakizishinikiza nchi barani humo kukabiliana na janga hilo la dhuluma kutoka kwa polisi ambazo aghalabu hukosa kuadhibiwa.
Chanzo: AFPE