Rais Zuma: Mauaji ya Marikana ni msiba wa kutisha
26 Juni 2015Katika hotuba yake juu ya ripoti ya tume iliyoundwa kuchunguza mauaji ya wachimbamigodi waliokuwa wanagoma yaliyofanywa na polisi tarehe 16 Agosti mwaka 2012, rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini amesema tume hiyo imebainisha kwamba maafisa wa polisi walifuata mpango uliokuwa na kasoro nyingi katika juhudi za kuwadhibiti wachimbamigodi hao.
''Tume, imegundua kwamba, operesheni ya polisi haikupaswa kufanywa jioni ya tarehe 16 Agosti, kutokana na kasoro katika mipango yao. Tume imebaini kwamba isingewezekana kuwanyang'anya silaha na kuwatawanya wachimbamigodi bila kumwaga damu nyingi.'' Amesema rais Zuma.
Rais Zuma amesema operesheni hiyo haukuwa na kuongozi kabisa , na baadhi ya polisi walionekana kutojua walichokuwa wanakifanya.
Tume iliyotoa ripoti hiyo yenye kurasa 600 iliundwa na serikali, ikiongozwa na Jaji mstaafu Ian Farlam, kuchunguza mauaji ya wachimbamigodi 34, na mengine ya watu 10 waliouawa wiki moja kabla
Polisi hawakujua cha kufanya
Ripoti hiyo imesema jeshi la polisi ndilo lenye lawama kubwa kuhusiana na mauaji hayo, kwa kukosa udhibiti wa hali ya mambo. Viongozi wa jeshi hilo pia wamekosolewa vikali na tume hiyo, kwa kukosa sifa za uongozi.
Kampuni ya Lonmin inayomiliki mgodi wa Marikana walikofanya kazi wachimbamigodi waliouawa pia imebebeshwa lawama, kwa kutochukua hatua za kutosha kuepusha mzozo. Chama cha kitaifa cha wachimbamigodi na wafanyakazi wa migodini pia kimeshutumiwa kwa kushindwa kuwadhibiti na kuwatuliza wanachama wake.
Lakini ripoti hiyo imewatakasa viongozi wa kisiasa, akiwemo makamu mwenyekiti wa chama tawala ANC Cyril Ramaphosa, ambaye wakati wa mauaji ya Maikana alikuwa mkurugenzi wa kampuni ya Lonmin na mwenye hisa katika kampuni hiyo. Rais Zuma amesema madai kwamba viongozi hao wanapaswa kuwajibishwa kwa vifo vya wachimbamigodi hayana msingi wowote.
Wachimbamigodi watilia shaka
Kuondolewa hatia viongozi hao hakukuwaridhisha wachimba migodi, kama alivyotangaza mmoja wao Johhanes Matladi, mfanyakazi wa kampuni ya Lonmin.
Amesema, ''Ramaphosa anahusika na mauaji yale, kwa sababu alituma barua pepe, na hata alizungumza kwa simu na watu wa Lonmin. Anajua fika kilichotokea, lakini siku moja ukweli utawekwa hadharani''.
Tume ya uchunguzi huo katika ripoti yake imependekeza kesi ya mauaji hayo ikabidhiwe kwa mwendeshamashitaka wa serikali ili ifanyiwe uchunguzi zaidi. Ripoti hiyo ilikabidhiwa kwa serikali tarehe 31 mwezi Machi, lakini serikali haikuiweka hadharani hadi pale iliposhinikizwa na vyama vya kiraia.
Mauaji hayo ya Marikana ndio kisa kibaya zaidi cha matumizi ya nguvu kupita kiasi kwa jeshi la polisi, tangu kumalizika kwa utawala dhalimu wa ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini.
Mwandishi: Daniel Gakuba/dpae/rtre
Mhariri: Abdu Mtullya