1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Polisi auawa kufuatia shambulizi Capitol Marekani

3 Aprili 2021

Mtu mmoja amepigwa risasi na kufariki baada ya kuvurumisha gari kwa maafisa wawili wa polisi karibu na majengo ya bunge nchini Marekani Capitol. Afisa mmoja wa polisi amekufa kufuatia kisa hicho.

USA I Kapitol in Washington abgeriegelt
Picha: J. Scott Applewhite/AP/picture alliance

Mshukiwa wa shambulizi hilo, alivurumisha gari dhidi ya maafisa wawili wa polisi waliokuwa wakishika doria katika majengo ya bunge ya Marekani yaliyoko Capitol mjini Washington DC, kabla ya kupigwa risasi na maafisa.

Shambulizi hilo limefanyika karibu na mahali ambapo wafuasi wa Donald Trump waliingilia majengo ya bunge na kuyavamia mnamo January 6 mwaka huu.

Kilichofanyika

Maafisa wa polisi wamesema gari hilo lililovurumishwa dhidi ya maafisa wa polisi liligonga vizuizi vya usalama, kisha mshukiwa aliyekuwa akiliendesha akatoka nje akiwa amebeba kisu mkononi na kukimbia kuelekea kwa maafisa wa polisi.

Gari lililovurumishwa wakati wa shambulizi kugonga polisi na vizuizi vya usalamaPicha: REUTERS

Mshukiwa huyo alikaidi amri kutoka kwa maafisa wa usalama na ndipo wakampiga risasi. Alifariki baadaye hospitalini.

Maafisa wawili waliohusika pia walikimbizwa hospitalini ambapo mmoja alifariki.

”Ni kwa masikitiko makubwa tunatangaza kuwa afisa wetu mmoja amefariki kutokana na majeraha,” amesema Yogananda Pittman, kaimu mkuu wa polisi wa Capitol.

Soma pia: Polisi aliyekabiliana na waandamanaji Marekani, afariki

Afisa aliyefariki alitambuliwa kuwa ni William ‘Billy' Evans.

”Tafadhali mkumbukeni kwenye maombi yenu,” amesema Pittman kwenye taarifa.

Kisa hicho kimetokea takriban mita 90 kutoka katika lango la Kaskazini la kuingia majengo ya bunge upande wa baraza la seneti, ambalo hutumika na maseneta pamoja na maafisa siku za kazi. Kwa sasa bunge liko likizoni.

Rais Biden asikitishwa na shambulizi pamoja na kifo cha afisa

Rais wa Marekani Joe Biden ambaye hayuko mjini Washington kwa sasa amesema  yeye pamoja na mke wake Jill Biden wamesikitishwa na shambulizi hilo.

Maafisa wa polisi wakishika doria katika maeneo ya majengo ya bunge Capitol.Picha: Erin Scott/REUTERS

"Jill pamoja na mimi tulisikitishwa kusikia kuhusu shambulizi katika eneo la kizuizi cha usalama kwenye majengo ya bunge ambalo limesababisha kifo cha afisa wa polisi William Evans wa kikosi cha polisi cha Capitol, na pia kusababisha afisa mwengine kulaza majeraha hospitalini," Biden amesema kwenye taarifa.

"Tunatuma salamu za rambirambi kwa familia ya Evans na yeyote anayehuzunika kufuatia kifo chake."

Maeneo hayo ya majengo ya bunge yamefungwa na usalama kuimarishwa. Maafisa wa usalama wamesema wameanzisha uchunguzi dhidi ya kisa hicho.