1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Polisi Iran yaendeleza ukandamizaji wa maandamano

11 Oktoba 2022

Iran imeimarisha msako wake katika maeneo ya wakaazi wa Kikurdi magharibi mwa nchi hiyo wakati maandamano yaliyochochewa na kifo cha mwanamke mwenye umri wa miaka 22 aliyekamatwa na polisi wa maadili yakipamba moto

Kanada Iran l Solidarität mit Mahsa Amini l Kunst und Protest in Vancouver
Picha: Mert Alper Dervis/AA/picture alliance

Polisi ya kuzima ghasia ilivamia kitongoji kimoja cha Sanandaj, ambao ni mji mkuu wa mkoa wa Kurdistan nchini Iran, wakati shirika la kimataifa la haki za binaadamu la Amnesty International na mshauri wa usalama wa kitaifa katika Ikulu ya White wakikosoa vitendo vya kuwashambulia waandamanaji waliokasirishwa na kifo cha Mahsa Amini.

Soma pia: Wanafunzi Iran, wafanyakazi wakaidi ukandamizaji wa maandamano

Kutoka mji mkuu Tehran, na kwingineko, video zimeibuka mitandaoni licha ya maafisa kuvuruga huduma za intaneti. Video jana zilionyesha wanafunzi wa vyuo vikuu na shule za sekondari wakiandamana na kuimba, huku baadhi ya wanawake na wasichana wakifanya matembezi bila ya vitaa kichwani au hijabu wakati maandamano hayo yakiingia wiki ya nne.

Ni wimbi kubwa la maandamano Iran katika miaka mitatuPicha: AFP/Getty Images

Shirika la Amnesty International limevikosoa vikosi vya usalama vya Iran kwa kutumia silaha za moto na kufyatua ovyo ovyo mabomu ya kutoa machozi, ikiwemo katika makazi ya watu. Limeuhimiza ulimwengu kuishinikiza Iran kusitisha ukandamizaji huo huku Tehran ikiendelea kuvuruga huduma za intaneti na mitandao ya simu za mkononi ili kuficha uhalifu wa wanaoufanya. Soma pia: Iran yawataka wageni kuheshimu sheria

Iran haijakiri maramoja kuhusu msako ulioanzishwa upya katika mji wa Sanandaj. Hata hivyo, Wizara ya Mambo ya Kigeni ya Iran ilimuita balozi wa Uingereza kuhusu hatua ya nchi hiyo kuwawekea vikwazo maafisa wa polisi ya maadili na usalama kutokana na ukandamizaji huo. Nasser Kanaani ni msemaji wa Wizara hiyo "Tunasimama kidete dhidi ya jaribio lolote la makundi mengine, hasa nchi za Magharibi ikiwemo Marekani, kutangaza vikwazo vipya au kuweka shinikizo ili tufikie makubaliano. Tunapinga hatua yoyote ya vikwazo dhidi ya watu wa Iran na serikali. Tutajibu vikali kwa wakati ufaao."

Amini alifariki akiwa mikononi mwa polisi IranPicha: Farouk Batiche/AA/picture alliance

Jake Suilivan, mshauri wa usalama wa kitaifa wa Rais wa Marekani Joe Biden, naye pia alisema ulimwengu unafuatilia kinachoendelea Iran.

Amini alikuwa Mkurdi na kifo chake kimesababisha hasira hasa katika eneo la Kikurdi la Iran, ambako maandamano yalianza Septemba 17 wakati wa mazishi yake. Serikali ya Iran inasisitiza Amini hakuteswa, lakini familia yake inasema mwili wake ulionyesha michubuko na dalili nyingine za kupigwa.

Soma pia: Khamenei azishtumu Marekani na Israel kwa machafuko Iran

Wakati huo huo, baadhi ya wafanyakazi wa sekta ya mafuta walijiunga na maandamano katika viwanda viwili muhimu jana, kwa mara ya kwanza wakiihusisha sekta muhimu kwa utawala wa Iran na machafuko hayo.

Maandamano hayo yanaweka changamoto kubwa kabisa kwa serikali ya Iran ya mfumo wa kidini tangu maandamano ya Vuguvugu la Kijani ya mwaka wa 2009.

AFP, AP

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW