1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Polisi Iran yafyatua risasi, dhidi ya waombolezaji wa Amini

27 Oktoba 2022

Maafisa wa usalama wa Iran wamefyatua risasi huku maelfu ya waombolezaji wakijitokeza katika mji wa Mahsa Amini aliyeuawa siku 40 zilizopita baada ya kukamatwa na polisi wa maadili wa Iran.

Iran I Zusammenstöße zwischen iranischen Sicherheitskräften und Demonstranten anlässlich des Todes von Mahsa Amini
Picha: UGC/AFP

Ni kulingana na wanaharakati pamoja na kanda za video ambazo zimethibitishwa. Katika tukio jingine watu wasiopungua 15 wameuawa kwenye shambulizi dhidi ya madhabahu takatifu ya waumini wa Kishia nchini humo. 

Amini aaliyekuwa na umri wa miaka 22, alifariki mnamo Septemba 26, siku tatu baada ya kukamatwa na polisi wa maadili wa Iran mjini Tehran, kwa madai ya kukiuka sheria inayowataka wasichana na wanawake wavae hijabu.

Polisi Iran yaendeleza ukandamizaji wa maandamano

Kifo chake kilizusha ghadhabu na wimbi la maandamano makubwa kuwahi kushuhudiwa nchini humo kwa miaka mingi. Maandamano hayo yaliongozwa na vijana wa kike kote nchini humo, huku wakichoma hijabu zao na kukabiliana na vikosi vya usalama.

Licha ya hatua za kiusalama kuimarishwa, waombolezaji waliojitokeza kwa makundi walimiminika katika mji wa Saqez, margharibi mwa nchi hiyo, kutoa heshima kwenye kaburi la Amini mwishoni mwa kipindi cha jadi cha maombolezo.

Maelfu zaidii ya waombolezaji wajitokeza kwenye kaburi la Mahsa Amini, ikiwa ni siku 40 tangu kifo chake.Picha: NNSRoj

Kwenye video iliyosambaa katika mitandao ya kijamii iliyohakikiwa na shirika la habari la AFP, kijana mmoja wa kike anaonekana akisimama juu ya gari bila hijab kichwani akitizama barabara iliyojaa waombolezaji na magari mengi.

Waandamanaji hao pia walipaza sauti wakisema "Kifo kwa dikteta", kabla ya baadhi yao kuonekana wakielekea katika ofisi ya gavana katikati ya mji huo. Vyombo vya habari vya Iran viliripoti kwamba baadhi yao walikuwa tayari kushambulia kambi ya kikosi cha usalama.

Shirika la kutetea haki za binadamu la Hengaw lenye makao yake Norway na ambalo hufuatilia visa vya ukiukwaji haki za binadamu katika majimbo ya Wakurdi, limesema vikosi vya usalama vilifyatua mabomu ya kutoa machozi na vilevile risasi dhidi ya waandamanaji katika viwanja vya Zindan na Saqez. Hata hivyo shirika hilo halikutoa maelezo ikiwa kuna watu waliouawa au waliojeruhiwa.

Katika tukio jingine nchini humo, watu wasiopungua 15 wameuawa kwenye shambulizi dhidi ya madhabahu moja muhimu ya dhehebu ya Shia kusini mwa Iran. Kundi linalojiita Dola la Kiislamu (IS) limedai kufanya shambulizi hilo.

Takriban watu 15 wauawa kwenye shambulizi dhidi ya waumini wa Kishia nchini Iran.Picha: Tasnim Agency

Shirika la habari linalomilikiwa na serikali limeripoti hayo na kuongeza kuwa shambulizi lilifanywa na gaidi aliyekuwa na silaha jana jioni wakati waumini walipokuwa wakiswali katika msikiti wa Shah Cheragh ulioko katika mji wa Shiraz. Watu wasiopungua 19 walijeruhiwa.

Ripoti za awali zilisema watu 13 waliuawa na 40 kujeruhiwa na kwamba wanamgambo watatu ndio walihusika kufanya shambulizi hilo.

Gavana wa eneo hilo Mohammad-Hadi Imanieh amekiambia kituo cha televisheni kinachomilikiwa na serikali kwamba mwanamgambo mwenye silaha alifyatua risasi kiholela dhidi ya waumini waliokuwa wakiswali.

Shambulizi hilo ni la pili mwaka huu dhidi ya dhehebu la waumini wa Shia nchini Iran, lakini ndilo shambulizi baya zaidi tangu shambulizi la Februari 2019 ambapo askari 27 wa intelijensia kutoka kikosi maalum cha Ulinzi wa Iran waliuawa kusini mashariki mwa nchi hiyo.

Mnamo Aprili, kijana mwenye umri wa miaka 21 mwenye asili ya Uzbek aliwachoma kisu viongozi wawili wa dini ya Shia hadi kufa katika msikiti wa kishia wa Imam Reza, na kumjeruhi muumini mwengine.

Shambulizi hilo lilijiri siku mbili baada ya viongozi wa kidini wa Sunni kupigwa risasi nje ya mji wa Gonbad-e Kavus.

(AFPE)

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW