1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Polisi Iraq wavamia kambi za waandamanaji

Yusra Buwayhid
26 Januari 2020

Maandamano ya Iraq yamekuwa yakiendelea kwa miezi kadhaa. Vikosi vya usalama sasa vinatumia nguvu dhidi ya waandamanaji. Kambi zao wamezichoma moto. Na hata vifo vimeshuhudiwa.

Irak Anti-Regierungs-Proteste in Bagdad
Picha: picture-alliance/AP Photo/H. Mizban

Watu wanne wameuawa katika maandamano ya Iraq yanayoendelea kwa miezi kadhaa katika taifa hilo lilotumbukia katika mzozo wa kisiasa na vurugu.

Vikosi vya kulinda usalama vimechoma moto mahema ya waandamanaji kusini mwa Iraq. Vikosi hivyo viliwatawanya waandamanaji kwa kutumia gesi ya kutoa machozi pamoja na risasi za moto katika viwanja viwili vya mji mkuu wa Baghdad ikiwamo cha Tahrir, na kusababisha kifo cha mtu mmoja, watu  wengine 44 walijeruhiwa.

Kwingineko watu watatu waliuawa kwa kupigwa risasi katika mji wa kusini wa Nasiriyah baada ya siku nzima ya makabiliano kati ya waandamanaji na vikosi vya usalama.

Waandamanaji wamejibu ukatili huo wa vikosi vya usalama kwa kuhamasisha watu kujitokeza kwa wingi zaidi barabarani.

Maandamano hayo ya kuipinga serikali yamepata pigo kubwa baada ya kiongozi wa kidini Muqtada al-Sadr na wafuasi wake pamoja na wanamgambo wanaomuunga mkono kujitenga na maandamano hayo. Wanaharakati wanahofia vuguvugu hilo la miezi minne litateseka zaidi baada ya kupoteza kinga ya kiongozi huyo wa Kishia.

Kiongozi wa Kishia awatenga waandamanaji

Al-Sadr ameamua kutounga tena mkono maandamano hayo baada ya maelfu ya wafuasi wake kufanya maandamano tofauti Ijumaa mjini Baghdad ya kutaka wanajeshi wa Marekani kuondoka nchini humo, ambayo waandamanaji wengi wanaoipinga serikali hawakushiriki. Msemaji wa Al-Sadr amesema waandamanji waliowatusi wafuasi wa kiongozi huyo wa Kishia.

Mwandamanaji wa vuguvugu la kuipinga serikali akiwa amejifunika uso mjini Baghdad, Jan.25, 2020.Picha: Getty Images/AFP/S. Arar

Kufuatia uamuzi huo wa al-Sadr Ijumaa, polisi wa kutuliza vurugu walichoma moto kambi za waandamanji mapema Jumamosi katika uwanja wa mji wa Basra kusini mwa Iraq, kulingana na wanaharakati wawili.

"Uwanja wa maandamano kwa sasa unadhibitiwa (na vikosi vya usalama), baada ya kutumia nguvu," amesema mwanaharakati Nakeeb Lueib. " `` Hii linazingatiwa kama usaliti na upande wa al-Sadr. ... Hakutakuwa na amani baada ya kile kilichotokea Basra jana usiku. ''

Katika uwanja wa Tahrir, ambako ndiko kitovu cha vuguvugu hilo la maandamano ya kuipinga serikali mjini Baghdad, waandamanaji wanasema wanahofia kitakachofuatia baadae.

"Tuko peke yetu sasa," amesema Mustafa, 24, ambae amakataa jina lake kamili kuandikwa kwa kuhofia usalama wake.

Waandamanaji hao wamekuwa wakiikosoa serikali kwa ufisadi, kiwango kikubwa cha ukosefu wa ajira pamoja na ushwaishi wa Iran ndani ya siasa za Iraq. Ukatili wa vikosi vya usalama umesababisha vifo vya waandamanaji wapatao 500 tangu Oktoba mosi.

"(Kauli ya al-Sadr) imesafisha njia kwa serikali kuukandamiza zaidi upinzani wa waandamanaji," amesema Hussein Ali, mwandamanaji mwenye umri wa miaka 35.

Wengine wanasema wataendelea kupambana. na wanayajenga tena mahema yao yaliyochomwa moto.

"Tumewatolea wito watu wengi zaidi kutuunga mkono katika uwanja wa Tahrir," anasema Noor, mwandamanaji wa kike ambaye hakutaka kutajwa kwa jina lake kamili.

Vyanzo: (ap,rtre)

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW