1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mshukiwa anayelaghai Wakenya kwenda vitani Ukraine adakwa

26 Februari 2026

Polisi nchini Kenya imemkamata mtu anayetajwa kuhusika katika mpango wa kuwarubuni Wakenya kwa ahadi za kazi nchini Urusi na baadaye kujikuta mstari wa mbele wa vita nchini Ukraine.

Kenya Nairobi 2026 | Familia za Wakenya ambao wanasadikiwa kuwa vitani Ukraine
Familia za Wakenya ambao wanasadikiwa kuwa vitani UkrainePicha: Andrew Kasuku/AP Photo/picture alliance

Polisi nchini Kenya imemkamata mtu anayetajwa kuhusika katika mpango wa kuwarubuni Wakenya kwa ahadi za kazi nchini Urusi na baadaye kujikuta mstari wa mbele wa vita nchini Ukraine.

Festus Omwamba amekamatwa kwa tuhuma za kujihusisha na biashara haramu ya binadamu katika mji wa Moyale kaskazini mwa Kenya, karibu na mpaka na Ethiopia, na atasafirishwa hadi mji mkuu, Nairobi.

Msemaji wa polisi ya Kenya Michael Muchiri amesema Omwamba ambaye alitambuliwa na wahanga watatu, alikamatwa wakati akijaribu kukimbia baada ya kurejea kutoka Urusi. Wiki iliyopita, serikali ya Kenya ilisema kuwa zaidi ya raia wake 1,000 waliajiriwa na Urusi kupigana vita nchini Ukraine.

Omwamba alikuwa hajulikani wapi aliko baada ya familia kuanza kupaza sauti kuhusiana na kupotea na vifo vya jamaa zao katika vita vya Ukraine.

Mama wa Kenya akionyesha picha ya mtoto wake aliyeko vitani UkrainePicha: Andrew Kasuku/AP Photo/picture alliance

Mbali na takwimu zilizotolewa na serikali za watu 1,000 kusadikiwa kuwa vitani Ukraine upande wa Urusi, lakini pia serikali ilitaja watu 39 wako hospitali, 28 hawajulikani walipo na 89 bado wako uwanja wa vita. Hadi sasa mtu mmoja tayari amethibitishwa kufa.

Kukamatwa kwa Omwamba ni hatua kubwa katika juhudi za serikali za kukomesha kuajiri Wakenya kupigana nchini Ukraine.

Waajiriwa wote walisema Omwamba alisimamia maombi yao ya visa ya watalii na ununuzi wa tiketi, na wiki mbili baada ya mawasiliano ya kwanza, walipokea visa na kusafiri hadi Urusi.

Taarifa za kijasusi za serikali ya Kenya

Ripoti ya kijasusi iliyowasilishwa kwa Bunge la Kenya na kiongozi wa walio wengi, Kimani Ichung'wah, ilisema maafisa wa serikali ya Kenya na Urusi walishirikiana na mashirika ya kuajiri wafanyakazi wakorofi ili kuwavutia Wakenya kwenye mstari wa mbele.

Mfungwa wa vita wa Kenya, Evans Kibet - Evans Kibet ni mwanariadha wa mbio za magari wa Kenya na yuko gerezani kwa wafungwa wa vita wa Urusi nchini Ukraine.Picha: DW

Hata hivyo, Ubalozi wa Urusi jijini Nairobi ulikana madai hayo,  ukisema katika taarifa Alhamisi iliyopita kwamba haujawahi kutoa visa kwa mtu yeyote anayekusudia kusafiri kwenda Urusi kupigana nchini Ukraine. Iliongeza kwamba, "Shirikisho la Urusi haliwazuii raia wa nchi za kigeni kujiandikisha kwa hiari katika jeshi."

Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya Musalia Mudavadi mnamo Februari 9 aliambia AP kwamba atasafiri kwenda Urusikwa kile alichokiita "mbinu ya kidiplomasia ya kudhibiti vyombo vyovyote vinavyotiliwa shaka vinavyomtumia mtu yeyote katika tukio hili baya."

Mudavadi aliongeza kuwa juhudi za kuhakikisha kuachiliwa huru kwa Wakenya walio katika magereza ya Ukraine na kuwarejesha nyumbani walioko Urusi zinaendelea.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW