1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Polisi wamuua mshukiwa wa "ugaidi" mjini Munich

Sylvia Mwehozi
6 Septemba 2024

Polisi wa Ujerumani hapo jana walimpiga risasi na kumuua kijana mmoja ambaye aliwafyatulia risasi katika kile walichokitaja kama "shambulio la kigaidi" lililozuiliwa katika ubalozi mdogo wa Israel wa mjini Munich.

Polisi wakiwa wamesimama nyuma ya gari la polisi Munich
Polisi wakiwa wamesimama nyuma ya gari la polisi MunichPicha: Matthias Schrader/AP Photo/picture alliance

Polisi wa Ujerumani hapo jana walimpiga risasi na kumuua mwanaume mmoja ambaye aliwafyatulia risasi katika kile walichokitaja kama "shambulio la kigaidi" lililozuiliwa katika ubalozi mdogo wa Israel wa mjini Munich.

Tukio hilo limetokea wakati wa kumbukumbu ya mauaji ya Michezo ya Olimpiki ya mwaka 1972. Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz alisema kupitia mtandao wa X kwamba polisi wa Bavaria huenda wamezuia jambo baya kutokea na kuongeza kuwa chuki dhidi ya Uyahudi na Uislamu hazina nafasi.

Watu 6 wajeruhiwa katika shambulio jipya la kisu Ujerumani

Polisi wamemtambua mwanaume huyo kuwa ni kijana mwenye umri wa miaka 18 na raia wa Austria mwenye mizizi ya Bosnia. Waziri wa mambo ya ndani wa Ujerumani Nancy Faeser alisema mwitikio wa haraka wa polisi wa Munich umemzuia mshambuliaji na pengine kuzuia kitendo cha kigaidi.

Polisi na waendesha mashtaka walisema siku ya Alhamisi kwamba walikuwa wakichunguza ikiwa lilikuwa ni jaribio la shambulio la kigaidi karibu na ubalozi mdogo wa Israel.

Magari ya polisi yakiwa yamefika kukabiliana na mshukiwa aliyeuawa karibu na ubalozi wa IsraelPicha: Magdalena Henkel/dpa/picture alliance

Polisi mjini Munich awali waliripoti operesheni kubwa katikati mwa jiji karibu na Ubalozi mdogo wa Israel, wakisema kuwa maafisa walimpiga risasi na kumgonga mshukiwa siku ya Alhamisi.

Polisi walisema saa chache baada ya tukio hilo kuwa mwanamume huyo alikuwa ni kijana wa miaka 18 mwenye uraia wa Austria lakini, wakati huo, hawakuzungumzia sababu za shambulio hilo wakisema uchunguzi unaendelea.

Soma: Scholz asema shambulizi la kisu Solingen ni ´ugaidi´

Mwandishi wa DW Lewis Sanders, akiripoti kutoka Munich alisema, "mamlaka za Austria zilitangaza kuwa mtu aliyefyatua risasi alikuwa akijulikana na alichunguzwa mwaka jana kwa tuhuma za itikadi kali na uhusiano na kundi la kigaidi."

Msemaji wa polisi alisema maafisa watano wamehusika katika makabiliano ya risasi na mtu huyo aliyekuwa akitumia silaha ya muda mrefu.

Video zinazosambaa mtandaoni, ambazo DW imeweza kuzithibitisha, zilionyesha kijana mdogo akiwa amebeba bunduki ya kizamani katika eneo hilo kabla ya kurushiana risasi na polisi.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW