1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mshairi wa Rwanda aliyetoweka ajiunga na waasi nchini Uganda

17 Februari 2022

Polisi nchini Rwanda imedai mshairi mmoja maarufu Innocent Bahati wa umri wa miaka 29 aliyetoweka nchini humo mwaka mmoja uliopita, amejiunga na kundi la waasi nchini Uganda

Ruanda Paul Kagame  Goma Kongo
Picha: Giscard Kusema

 

Bahati ambaye amekuwa akichapisha mashairi katika mtandao wa You Tube, amekuwa hajulikani alipo tangu Februari 17 mwaka jana na kuibua wasiwasi miongoni mwa makundi ya kutetea haki ambayo  yanasema nafasi ya uhuru wa kujieleza katika taifa hilo la Afrika Mashariki linalodhibitiwa vikali inazidi kupungua.

Lakini siku ya Jumatano, Ofisi ya Upelelezi ya Rwanda (RIB) ilisema kwamba Bahati, ambaye kazi yake ililenga masuala ya kijamii, alivuka mpaka na kuingia Uganda na kujiunga na kundi la waasi. Msemaji wa RIB Thierry Murangira, amesema kwamba mara kadhaa, Bahati alivuka na kuingia nchini Uganda kupitia maeneo ya mipaka isiyo rasmi ambapo alikutana na maafisa wa usalama wa Uganda na makundi yanayoipinga Rwanda.

Murangira pia amekiambia kituo cha habari cha mtandaoni kinachojulikana kama Taarifa kwamba pia imebainishwa Bahati anashirikiana na watu wanaoipinga serikali ya Rwanda wenye makao yao nchini Ubelgiji na Marekani ambapo anapokea msaada wa kifedha. Awali, shirika la Human Rights Watch lilisema kuwa kutoweka kwa Bahati kunapaswa kutiliwa shaka kutokana na kuzuiliwa kwake awali kwa kuikosoa serikali ya rais Paul Kagame.

Waandishi 100 wamuandikia Rais Kagame barua wazi

Wiki iliyopita, zaidi ya waandishi 100 ikiwa ni pamoja na mshindi wa tuzo ya riwaya kutoka Canada, Margeret Atwood, waliandika barua wazi kwa Kagame wakielezea wasiwasi wao na kumtaka aingilie kati katika kumtafuta Bahati.

Barua hiyo ilisema kwamba wanamuandikia rais huyo kwasababu ya miito ya awali ya kumhimiza aingilie kati katika swala hilo la Bahati na kwa maslahi ya haki yake ya maisha. Barua hiyo iliendelea kusema kuwa ushairi sio uhalifu na dunia inasubiri kusikia tena sauti ya Innocent Bahati .

Murangira amesema wakosoaji hawakukabiliwa na kikwazo cha kuzungumza dhidi ya serikali nchini Rwanda. Pia ameongeza kuwa haoni sababu ya ukosoaji wa serikali kuwa tatizo na kwamba  watu wengi nchini Rwanda huchapisha habari za kuikosoa serikali katika majukwaa tofauti akisema ni haki yao ya kikatiba kuelezea maoni yao kuhusu kile serikali inachokifanya.

Rwanda imekuwa ikishtumiwa kwa ukiukaji wa haki

Nchi hiyo, inayotawaliwa na Kagame tangu kumalizika kwa mauaji ya halaiki ya 1994 ambayo yalisababisha vifo vya watu 800,000 hasa watutsi, mara nyingi imekuwa ikishutumiwa kwa ukiukaji wa haki, huku wakosoaji wa serikali wakifungwa jela na vyombo huru vya habari pia vikifungiwa.

Mpinzani mmoja wa Rwanda ambaye alitumia mtandao wa YouTube kuikosoa serikali alihukumiwa kifungo cha miaka saba jela mnamo mwezi Novemba mwaka jana baada ya kupatikana na hatia ya kughushi na kujifanya kuwa mtu tofauti.

Dieudonne Niyonsenga, ambaye anajulikana katika mtandao wa You Tube kama Cyuma kumaanisha chuma alifahamika kwa kuzungumzia ukiukaji wa haki za binadamu katika kituo chake cha televisheni cha Ishema ambacho kilikuwa kimewavutia watazamaji milioni 15. Kufungwa kwake, kunatokea wiki kadhaa baada ya mtumiaji mwengine maarufu wa YouTube Yvonne Idamange kuhukumiwa miaka 15 jela kwa kuchochea vurugu kupitia mtandaoni.

 

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW