1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Polisi Msumbiji wafyatua mabomu ya machozi kutawanya raia

21 Oktoba 2024

Polisi nchini Msumbiji wamefyatua mabomu ya kutoa machozi kuutawanya umati mdogo wa watu mjini Maputo. Maduka katika mji huo yamefungwa kutokana na maandamano yaliyopangwa kupinga udanganyifu katika uchaguzi.

Maandamano Msumbiji
Maandamano MsumbijiPicha: Romeu da Silva/DW

Polisi nchini Msumbiji wamefyatua mabomu ya kutoa machozi kuutawanya umati mdogo wa watu mjini Maputo. Maduka katika mji huo yamefungwa kutokana na maandamano yaliyopangwa kupinga udanganyifu katika uchaguzi.

Vidio zilizochapishwa mitandaoni zimewaonesha watu kadhaa wakiwemo waandishi wa habari wakisambaa baada ya polisi waliojihami kwa silaha kuingia mitaani. Mwandishi wa shirika la AFP aliyekuwa eneo la tukio pia aliripoti kuhusu tukio hilo.

Kiongozi wa upinzani Venancio Mondlane, aliyewania urais katika uchaguzi wa Oktoba 9, aliitisha maandamano kupinga matokeo ya mapema. Matokeo hayo yalionyesha chama tawala cha Frelimo kikiongoza.

Vurugu zilizuka baada ya washirika wawili wa kiongozi huyo kupigwa risasi na kuuawamjini Maputo siku ya Jumamosi. Wakili Elvino Dias na Paulo Guambe, mgombea kutoka chama kidogo cha Podemos walikuwa katika gari wakati walipozingirwa na magari mengine na kisha kupigwa risasi.