Polisi Myanmar yatumia vitoa machozi dhidi ya waandamanaji
26 Februari 2021Mtu mmoja amejeruhiwa katika makabiliano hayo ya polisi na waandamanaji mjini Yangon, huku watu wengine kadhaa wakijeruhiwa katika mji mwengine wa Mandalay hii ikiwa ni kwa mujibu wa walioshuhudia.
Polisi hadi sasa haijatoa tamko lolote kuhusu makabiliano hayo.
Taifa hilo la kusini mwa Asia limekuwa katika mgogoro mkubwa tangu jeshi lilipochukua madaraka mnamo Februari Mosi, na kumuweka kizuizini kiongozi wa serikali, Aung San Suu Kyi, na wanachama kadhaa wa chama chake cha NLD, baada ya jeshi kulalamika kuwa uchaguzi wa Novemba uliokipa ushindi chama cha Suu Kyi ulikumbwa na udanganyifu.
soma zaidi: G7 wataka ukandamizaji ukome Myanmar
Lakini tume ya uchaguzi inasisitiza uchaguzi ulikuwa wa haki.
Tovuti moja ya Myanmar ikiwanukuu maafisa wa chama cha Kyi cha NLD, imesema kiongozi huyo wiki hii aliondolewa katika kifungo cha nyumbani mjini Naypytaw na kupelekwa katika eneo lisilojulikana. Awali, wakili wake alilalamika kutopewa nafasi ya kumfikia mteja wake kuelekea Machi Mosi anayotarajiwa kufikishwa mahakamani.
Waandamanaji wasema wataendelea kupigania demokrasia
Kwa zaidi ya wiki tatu Myanmar imeshuhudia maandamano ya kila siku pamoja na migomo inayofanywa na watu wanaounga mkono demokrasia. Mjini Yangon, mamia ya watu walikusanyika katika makundi madogo madogo kabla ya kuwatawanya na polisi.
Watu wengi walikamatwa akiwemo muandishi habari mmoja kutoka Japan, lakini baadaye aliachiliwa. Hiyo ilikuwa ni mara ya kwanza mwanahabari kutoka nje kukamatwa na polisi ya Mnyanmar tangu maandamano yalipoanza.
Kiongozi wa jeshi, Jenerali Min Aung Hlaing, amesema jeshi lake limekuwa likitumia nguvu ya wastani dhidi ya waandamanaji, lakini waandamanaji watatu wanasemekana kuuwawa ingawa polisi nayo imejibu kwa kusema afisa wake mmoja aliuwawa katika maandamano yanayoendelea tangu Februari Mosi.
soma zaidi: Umoja wa Mataifa walaani matumizi ya nguvu Myanmar
Jeshi limeahidi uchaguzi mpya lakini bado haijatoa tarehe rasmi ya kufanyika kwa mchakato huo.
Kwa sasa uchaguzi hautafanyika hadi baada ya kumalizika kwa kipindi cha hali ya dharura cha mwaka mmoja kilichowekwa na jeshi lilipompindua kiongozi wa kiraia, Aung San Suu Kyi.
Vyanzo: reuters/afp