1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu kadhaa wauwawa kwa kupigwa risasi Marsabit

14 Agosti 2024

Watu wanane wameuawa kwa kupigwa risasi kabla ya miili yao kuteketezwa kwa moto eneo la Forolle mpakani mwa Kenya na Ethiopia katika jimbo la Marsabit.

Kenya
Mkutano wa maafisa wa usalama na wakaazi wa Marsabit wanaotaka usalama kuimarishwa katika eneo hilo la Kaskazini mwa Kenya Picha: Michael Kwena/DW

Wakaazi wanaoishi katika mpaka wa Kenya na Ethiopia katika jimbo la Marsabit, wanaitaka wizara ya usalama wa ndani kuwapa maafisa wa polisi wa akiba bunduki zaidi ili kuwasaidia polisi kulinda mpaka huo. Wito huo unafuatia kisa ambapo lori lililokuwa limebeba watu kumi kutoka Mjini Marsabit kuelekea Dukana, kushambuliwa na watu waliokuwa na silaha kabla ya kuteketezwa kwa moto ndani ya lori hilo. 

Katika tukio hilo, watu wawili walinusirika kifo na mmoja kati yao anaaendelea kupokea matibabu.

Kwa upande mwingine, baadhi ya viongozi wa Marsabit wanadai washambuliaji hao wanatokea Ethiopia.
Kwa mujibu wa mwakilishi wadi wa Turbi Galgallo Huka na seneta wa jimbo la Marsabit Mohammed Chute, tukio hilo linapaswa kuchunguzwa kwa kina.

Akithibitisha kisa hicho, naibu kamishna wa Turbi Daniel Ouma amesema kwamba, maafisa wa upelelezi wameanzisha uchunguzi kuhusu tukio hilo kando na kuimarisha usalama kwenye barabara hiyo ya mpakani.

“Tumeweka maafisa wa jeshi wakishirikiana na askari wetu na tunauhakika usalama utapatikana,” alisema Turbi Daniel Ouma

Katika kipindi cha wiki mbili sasa, watu wenye silaha wanaodaiwa kutoka Ethiopia wameshambulia Kenya zaidi ya mara tatu huku wakimuua afisa mmoja wa polisi na kuwateka nyara watu wawili.

Mwandishi: Michael Kwena