1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Polisi Rwanda yamchunguza mkosoaji wa Kagame

Sylvia Mwehozi
30 Agosti 2017

Polisi nchini Rwanda wamesema hii leo wanamchunguza Diane Shima Rwigara ambaye ni mkosoaji wa Rais Paul Kagame na ambaye aliondolewa katika kinyang'anyiro cha urais mapema mwezi huu kwa ukwepaji wa kodi na udanganyifu. 

Ruanda Diane Rwigara
Picha: Getty Images/AFP/C. Ndegeya

Msemaji wa polisi Theos Badege amesema maafisa wamefanya upekezi nyumbani kwa familia ya Rwegara katika mji mkuu wa Kigali, na kukanusha taarifa zilizosambaa mtandaoni kwamba amekamatwa. Badege anasema "Rwigara hayuko chini ya ulinzi wa polisi. Kinachoendelea ni uchunguzi juu ya mashtaka mawili. Moja ni udanganyifu unaohusishwa moja kwa moja na Diane Rwigara binafsi na mwingine ni kukwepa kodi ambayo inahusu familia. Jana tulifanya upekezi ulioruhusiwa kwa kibali kilichotolewa na waendesha mashtaka lakini pia waliitwa kwa ajili ya kuhojiwa polisi. Baadhi ya vifaa vyao vya kielektroniki kama wao kama simu na kompyuta viko mikononi mwa polisi."

Diane Shima Rwigara katika mkutano na waandishi wa habari Mei 3Picha: Getty Images/AFP/C. Ndegeya

Rwigara mwenye miaka 35 ambaye ni mhasibu wa zamani amemshutumu mara kwa mara Kagame kwa udhalilishaji mbaya na kukosoa chama chake cha Rwanda Patriotic Front kwa kung'ang'ania madaraka.

Tume ya uchaguzi ilimuondoa Diane katika kinyang'anyiro cha urais wa mwezi huu, ikisema kwamba hakuwasilisha saini za wafuasi wake za kutosha na kwamba baadhi ya majina aliyotuma yalikuwa ya watu waliokufa, madai ambayo aliyakanusha.

Wizara ya mambo ya nje ya Marekani na Umoja wa Ulaya walikosoa uamuzi huo wa kumuondoa katika mbio za urais ambazo zilishuhudia Rais Kagame akichaguliwa tena kwa asilimia 98.8 ya kura.

Polisi wamesema leo Jumatano kwamba wamefanya upekuzi katika nyumba ya Rwigara baada ya kupokea nyaraka kutoka kwa tume ya uchaguzi hata hivyo hawakutoa taarifa za kina.

Simu ya Rwigara na za ndugu zake watatu zilikuwa zimezimwa siku ya leo Jumatano wakati mwandishi wa shirika la habari la Reuters lilipojaribu kuwapigia. Mwandishi wa Reuters alipojaribu kwenda nyumbani kwa mwanamke huyo hakuna aliyefungua mlango.

Msemaji wa polisi anasema madai ya ukwepaji wa kodi yanachunguzwa kwa ushirikiano na mamlaka ya kodi nchini Rwanda.

Rais wa Rwanda Paul KagamePicha: Picture alliance/AP Photo/E. Murinzi

Kamishina wa mamlaka hiyo Richard Tusabe amesema kampuni ya tumbaku ya familia ya Rwigare haijalipa kodi kwa kipindi cha miaka mitano. Hakuna ndugu wa familia aliyepatikana kuthibitisha taarifa hizo.

Kagame amepata sifa kimataifa kwa kurejesha uchumi nchini Rwanda tangu mauaji ya kimbari yam waka 1994, wakati watu 800,000 wengi wakiwa Watusi na wachache wahutu walipouawa.

Lakini pia amepata ukosoaji mkubwa kwa kile makundi ya haki za binadamu yanasema ni kuenea kwa ukiukwaji, mbinyo kwa vyombo vy ahabari vya binafsi na ukandamizaji wa upinzani.

Rwigara ni binti wa hayati Assinapol Rwigara,  ambaye alianguka dhidi ya Kagame kabla ya kifo chake katika ajali ya gari mwaka 2015. Kagame amekuwa rais wa Rwanda tangu kumalizika kwa mauaji ya kimbari ya 1994 .

Mwandishi: Sylvia Mwehozi/Reuters

Mhariri: Iddi Ssessanga