1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Polisi Sri Lanka yaamrishwa kuwafyatulia risasi waandamanaji

11 Mei 2022

Polisi ya Sri Lanka imeamrishwa kukabiliana na waandamanaji kwa kutumia risasi za moto ili kuzuia uvunjaji wa sheria.

Sri Lanka I Proteste in Colombo
Picha: Ishara S. Kodikara/AFP/Getty Images

Haya yamesemwa na afisa mmoja mwandamizi katika serikali ya nchi hiyo wakati ambapo magari ya kivita na wanajeshi wakiwa wameonekana katika mitaa ya mji mkuu Colombo.

Haya yote yanafanyika siku mbili baada ya waandamanaji wanaoiunga mkono serikali kuwashambulia waandamanaji wengine waliokuwa wanaandamana kwa amani hatua iliyoibua wimbi la machafuko kote nchini humo.

Amri ya kuwapiga risasi wanaoshiriki katika vitendo hivyo vya machafuko imetolewa wakati ambapo visa vya uchomaji moto na uharibifu wa biashara vimeshuhudiwa licha ya marufuku ya kutotoka nje iliyoanza kutekelezwa usiku wa Jumatatu.

Magari ya kijeshi yaondoka Colombo

Lakini marufuku hiyo ya kutotoka nje inaonekana kupuuzwa na waandamanaji kwani hoteli moja inayodaiwa kumilikiwa na jamaa mwenye uhusiano na rais wa nchi hiyo Gotabaya Rajapaksa, ilichomwa moto usiku wa kuamkia Jumatano.

Waandamanaji wanaoiunga mkono serikali wakimshambulia mwandamanaji mpinzaniPicha: Buddhika Weerasinghe/Getty Images

Polisi inasema watu wanane wamefariki dunia tangu Jumatatu kufuatia maandamano hayo yaliyosababishwa na hali mbaya ya kiuchumi nchini Sri Lanka.

Video zilizochapishwa kwenye mitandao ya kijamii zimeonyesha magari ya kijeshi yakiondoka mji mkuu na wanajeshi wakiweka vizuizi katika sehemu tofauti kote nchini humo huku kukiwa na hofu kwamba pengo la kisiasa huenda likapelekea jeshi kuchukua madaraka.

Ila afisa mwandamizi katika wizara ya ulinzi Kamal Gunaratne katika kikao na waandishi wa habari kilichofanywa pamoja na wakuu wa jeshi, amekanusha madai ya jeshi kuchukua madaraka, akidai hakuna mwenye nia ya kufanya hivyo kwa kuwa hilo halijawahi kufanyika nchini humo.

Gunaratne amesema jeshi litarudi kambini mara tu hali itakapotengemaa. Rais Rajapaksa mwenyewe ni afisa mkuu wa jeshi na ndiye waziri rasmi wa ulinzi.

Upinzani hautofanya kazi na Rajapaksa

Jumatano waandamanaji wameonekana kukita kambi nje ya afisi ya rais huku wakisema wanataka ukoo mzima wa Rajapaksa uondoke katika uongozi wa nchi hiyo kutokana na ufisadi.

Kifaru cha jeshi katika mitaa ya ColomboPicha: Eranga Jayawardena/AP/picture alliance

Lakini katika ujumbe aliouandika kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter, Rajapaksa ametoa wito kwa raia wa Sri Lanka kuungana ili kuzimaliza changamoto za kiuchumi, kijamii na kisiasa zinazoikumba nchi hiyo.

Chama kikuu cha upinzani SJB kwa mara nyengine tena kimesema hakitokuwa sehemu ya serikali yoyote inayoongozwa na Rajapksa kama rais hata baada ya nduguye Mahinda kuachia ngazi kama waziri mkuu hapo Jumatatu.

Umoja wa Ulaya umetoa wito kwa serikali nchini humo kuanzisha uchunguzi kuhusiana na yanayoendelea na kuwachukulia hatua wanaochochea machafuko.

Sri Lanka inaelekea kufilisika baada ya kusema kwamba inasimamisha ulipaji wa mikopo ya kigeni ya kima cha dola bilioni 7 ambayo ilikuwa inatakiwa kuilipa mwaka huu. Jumla ya deni lake ni dola bilioni 51.