1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Polisi Tanzania yawashikilia viongozi wa upinzani

3 Novemba 2020

Polisi nchini Tanzania imewakamata viongozi kadhaa wa upinzani kwa madai ya kupanga maandamano yasio na kibli, baada ya kukituhumu chama tawala CCM kwa kufanya udanganyifu kwenye uchaguzi mkuu

Tansania Opposition Freeman Mbowe
Picha: Emmanuel Herman/REUTERS

Viongozi wa upinzani Tanzania wamesema kuwa polisi waliwakamata wenzao kadhaa jana na kuwashitaki kwa makosa yanayohusiana na ugaidi. Na kwamba walifunga maeneo yote ambayo maandamano ya amani yalipaswa kufanyika, kufuatia uchaguzi wa wiki jana waliosema ulijaa dosari.

Miongoni mwa waliokamatwa ni pamoja na aliyekuwa mgombea wa urais kupitia chama cha Chadema Tundu Lissu, lakini akaachiliwa baadaye. Hayo ni kulingana na Katibu Mkuu wa chama cha Chadema John Mnyika. Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe pia alitiwa mbaroni.  Kulingana na Chadema, jumla ya vigogo wake 20 wanashikiliwa na polisi.

Kamanda wa kanda maalumu ya Dar es Salaam Lazaro Mambosasa aliwathibitishia waandishi wa habari mjini Dar es Salaam jana Jumatatu kwamba hawakutoa kibali chochote cha kuruhusu maandamano kwa hivyo wito wao kwa vijana kuandamana ni kinyume cha sheria.

Ukamataji huo unajiri baada ya vyama viwili vikuu vya upinzaninTanzania kuitisha maandano makubwa yasiyo kikomo, kufuatia matokeo ya uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 28. Vyama hivyo vilipinga matokeo yaliyotangazwa.

Mbowe na wapinzani wengine wanazuiliwa na polisiPicha: DW/F. Nwaka

Taarifa ya pamoja iliyotolewa jana jioni na Tundu Lissu pamoja na kiongozi wa ACT Wazalendo Zitto Kabwe ilisema kuwa Freeman Mbowe na viongozi wengine wawili wa Chadema sasa wanakabiliwa na mashtaka yanayohusiana na ugaidi, kumaanisha hawaruhusiwi kuachiliwa huru kwa dhamana. Taarifa hiyo ya pamoja pia imeeleza kuwa wanachama wa ACT Wazalendo wangali wanashikiliwa na polisi visiwani Zanzibar.

Wamezitaka nchi nyingine kuikemea serikali ya Tanzania kwa matendo yake ya kiimla huku wakisisitiza kuwa maandamano yataendelea.

Mkuu wa kampeni ya chama cha ACT Wazalendo Emmanuel Mvula ameliambia shirika la Habari la Associated Press kwamba kumekuwa na maafisa wengi wa vikosi vya usalama katika mji mkuu wa kibiashara Dar es Salaam, ambapo vyama viwili vikuu vya upinzani vilipanga kuandamana hadi katika makao ya Tume ya Uchaguzi.

Kulingana na matokeo yaliyotangazwa na tume ya uchaguzi, Rais John Magufuli alipata ushindi mkubwa wa asilimia 84 ya kura zilizopigwa, huku mgombea wa upinzani Tundu Lissu akipata asilimia 13 pekee ya kura. Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania, umesema kumekuwepo madai ya kuaminika kuhusu dosari kwenye uchaguzi huo pamoja na vitisho.

Aidha Umoja wa Ulaya ulielezea wasiwasi wake jana kuhusu dosari zilizoripotiwa. Kwenye taarifa, Umoja huo ulisema madai hayo mazito yana athari kuhusu uwazi na uaminifu kwa ujumla wa mchakato mzima, na kwamba yanapaswa kushughulikiwa kisheria.

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola Patricia Scotland naye ameelezea wasiwasi wake kuhusu ripoti za machafuko na za visa vya udanganyifu wakati wa uchaguzi huo.

(DPAE, APE)