Polisi Uganda wamchunguza aliyekutwa na kichwa cha mtu
15 Septemba 2020Kisa hicho kimewashtua watu mbalimbali wakikielezea kuwa kitendo cha ushirikina ambacho sababu za kufanyika kwake zinatakiwa kuchunguzwa ipasavyo. Kulingana na taarifa za awali, mwanamume huyo ambaye inasemekana alijifanya kuwa msichana aliwasili kwenye lango la majengo ya bunge na kutaka kuwasilisha zawadi ya spika wa bunge.
Kutokana na hali ya wasiwasi aliyokuwa nayo, walinzi walimshuku na kumhoji zaidi huku wakitaka kuiona zawadi yenyewe. Walipigwa na mshtuko mkubwa walipogundua kuwa zawadi ya spika ilikuwa kichwa cha binadamu aliyekadiriwa kuwa mtoto mwenye umri wa chini ya miaka mitano.
Naibu Msemaji wa polisi Kanda ya Mji wa Kampala Luke Owoyesigire, amesema kwa sasa polisi wanachunguza kama kichwa hicho ni cha kiwiliwili cha mtoto kilichopatikana katika kichaka mjini Masaka, umbali wa kilomita 130 hivi kutoka kwenye mji mkuu, Kampala siku ya Jumatatu asubuhi.
Kisa hicho cha mtu kuwasilisha kichwa cha mtu kwenye majengo ya bunge ndiyo gumzo linalotawala kwa sasa mjini Kampala na sehemu mbalimbali za nchi. Huku wengine wakidhani kuwa ni mojawapo ya visa vya kafara za watoto zinazofanywa kila mara na baadhi ya watu wanaoendekeza imani za ushirikina, baadhi wana mtazamo kuwa kimelengwa kumweka spika wa bunge katika fedheha katika kipindi hiki cha uchaguzi.
Ijapokuwa aliweza kushinda katika uchaguzi wa halmashauri kuu ya chama tawala, Spika wa Bunge Rebecca Kadaga alikabiliwa na upinzani tofauti na hapo awali. Lakini matukio ya watu kushiriki vioja kwenye majengo ya bunge la Uganda yameshuhudiwa mara kadhaa. Kuna wakati kundi la vijana liliwaleta na kuwatupa kwenye lango la bunge nguruwe wadogo wakiwa wamepakwa rangi ya njano ya chama tawala. Maandamano kadhaa yaliyo kinyume na sheria hufanywa na wahusika kutaka kuwasilisha malalamiko na vilio vyao kwa spika wa bunge.
Visa vya kafara za watu navyo huripotiwa kila mara na washukiwa kadhaa wako gerezani kuhusiana na madai hayo. Polisi wamefichua kuwa mshukiwa huyo atapimwa kufahamu hali yake ya akili, lakini pia kujua kama kuna wahusika wengine katika kisa hicho ambacho kimewastajabisha wengi. Hadi kufikia wakati wa kuandaa taarifa hii, ofisi ya spika haikuwa imetoa taarifa yoyote kuhusu kisa hicho.