Polisi Ujerumani wawahamisha wanaharakati kupisha mgodi
11 Januari 2023Awali, polisi ilishatangaza kwamba Jumatano (Januari 11) ingelikuwa siku ya kuwahamisha mamia ya wanaharakati ambao wamekuwa wakikusanyika hapo kwa miezi kadhaa.
Polisi waliwasili mapema asubuhi kwenye eneo hilo kutekeleza uamuzi huo wakiwa na mavazi na zana za makabiliano.
Hata hivyo, kupitia mtandao wa Twitter, jeshi la polisi liliwatumia ujumbe wanaharakati hao likiwataka "kutumia njia za amani" kuelezea msimamo wao na "sio nguvu na machafuko."
Soma zaidi: Ujerumani na India kushirikiana kulinda mazingira
Polisi walianza operesheni yao kwa kuzungushia uzio eneo hilo na kuwataka wanaharakati kuondoka wenyewe "kabla ya kuchukuliwa hatua za kisheria."
Wanaharakati waweka vizuizi
Kwa mujibu wa mwandishi wa shirika la habari la dpa, wanaharakati wapatao 100 waliweka vizuizi na kutumia kila walichonacho kuzuia kuhamishwa kwenye eneo hilo, yakiwamo mawe.
Kampuni kubwa ya nishati, RWE, inadhamiria kukibomoa kijiji hicho ili ichimbe madini ya lignaiti, aina ya makaa ya mawe yenye rangi ya kahawia.
"Leo, RWE Power itaanza kuyabomoa makaazi ya zamani ya Luetzerath. Tunawaomba wavamizi kutekeleza amri ya utawala wa sheria na kukomesha ukaliaji haramu wa majengo, miti na maeneo yanayomilikiwa na RWE kwa amani." Ilisema taarifa iliyotolewa na kampuni hiyo siku ya Jumatano.
Soma zaidi: COP27: Mataifa makubwa yaunda muungano wa nishati ya upepo
Siku ya Jumanne (Januari 10), waandamanaji walikataa kutii amri ya mahakama inayowapiga marufuku kuwapo kwenye eneo hilo.
Badala yake, baadhi yao walichimba mahandaki na kuweka vizuizi vya kuzuia magari makubwa kukifikia kijiji hicho, kabla ya polisi kuwarudisha nyuma kwa nguvu.
Hatari kwa mazingira
Wengi wa wakaazi halisi wa eneo hilo walishahama na ardhi hiyo sasa ni mali ya RWE, lakini wanaharakati wameyakalia majengo kadhaa kwa miezi mingi na idadi yao imekuwa ikiongezeka katika wiki za hivi karibuni.
Walinzi wa mazingira wanasema kukiangamiza kijiji hicho kwa lengo la kutanuwa mgodi wa makaa ya mawe wa Garzweiler kutasababisha kiwango kikubwa cha uzalishaji wa gesi chafu.
Soma zaidi: Uhaba wa nishati: Wajerumani wataka serikali kusaidia
Kwa upande wao, serikali pamoja na kampuni ya nishati ya RWE wanasema makaa hayo yanahitajika kuhakikisha Ujerumani ina nishati ya kutosha.
Kampuni ya RWE ilifikia makubaliano na serikali mwaka jana yanayoruhusu kijiji hicho kubomolewa kwa masharti ya kukomesha matumizi ya makaa ya mawe ifikapo mwaka 2030 badala ya 2038.
Watetezi wa mazingira wanasema makubaliano hayo yanakwenda kinyume na wajibu wa Ujerumani kwa ahadi yake ya kupunguza uzalishaji wa gesi chafu.
"Hoja ya serikali na RWE ni kinyume na utafiti unaothibitisha kuwa makaa ya mawe kutoka kijiji cha Luetzerath hayatahitajika kukabiliana na hali ya sasa ya ukosefu wa nishati", kwa mujibu wa wanaharakati hao.
Vyanzo: AP, dpa