Raia wawili wa Kosovo watiwa mbaroni Ujerumani
23 Desemba 2016Maafisa wa polisi waliokuwa wamevalia sare za jeshi hilo na wale ambao walikuwa katika mavazi ya kawaida wakiwa na silaha waliwatia mbaroni watu wawili baada ya kuvamia eneo la maduka la Oberhausen na kufanya msako katika eneo hilo lililoko katika jimbo la North Rhine- Westphalia
Kwa mujibu wa taarifa za kipolisi wanaume hao wawili ambao ni ndugu wazaliwa wa Kosovo wenye umri wa miaka 28 na 31 wanashukiwa kutaka kufanya shambulizi katika eneo hilo la maduka ikiwa ni pamoja na eneo maalumu la soko la Krismasi lililoko kwenye maduka hayo.
Maafisa wa usalama nchini Ujerumani wanasema walifanya msako katika maeneo kadhaa mjini Berlin na katika maeneo mengine kwa lengo la kumtia mbaroni Anis Amri mwenye umri wa miaka 24 anayehusishwa na shambulizi la lori mjini Berlin lililoua watu 12 katika soko la Krisimasi mjini Berlin Jumatatu wiki hii.
Amri anadaiwa kufikia katika eneo lililoko katika jimbo la North Rhine- Westphalia wakati alipokuwa akitafuta hifadhi ya kuishi nchini Ujerumani katikati ya mwaka 2015.
Kansela Angela Merkel aonyesha matumaini ya kukamatwa haraka mshukiwa wa shambulizil la Berlin
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amesema ana matumaini ya kukamatwa haraka mshukiwa huyo na kuongeza kuwa ametiwa moyo na jinsi watu wengi nchini ujerumani walivyoonekana kuguswa na shambulizi hilo.
Gazeti moja la nchini Ujerumani la "Bild" limeripoti hii leo kuwa watu watatu miongoni mwa 12 waliouawa katika shambulizi hilo bado hawajatambuliwa.
Waliotambuliwa ni raia sita wa ujerumani, raia mmoja wa Israel, raia mmoja wa Italia pamoja na raia wa Poland ambaye ni dereva la lori hilo lililokuwa na shehena ya bidhaa zilozukuwa zikitarajiwa kupakuliwa nchini Ujerumani.
Ama kwa upande mwingine maafisa wa usalama nchini Ujerumani wanasema walifanya msako katika basi lililokuwa limebeba watalii katika mji wa Heilbronn katika jimbo la kusini la Baden- Wurttemberg. hata hivyo maafisa hao wanasema hakuna mtu aliyekamatwa kutokana na msako uliofanywa kwenye basi hilo.
Mikanda ya vidio ya tangu jumatatu iliyopita ambayo taarifa zake zimechapishwa na vyombo kadhaa vya habari nchini Ujerumani inaonyesha kuwa mshukiwa wa shambulizi hilo Anis Amri alitoweka mara tu baada ya kulibamiza lori hilo katika soko la Krismasi mjini Berlin.
Chombo cha habari cha matangazo cha umma cha RBB cha mjini Berlin kimeripoti kuwa picha zilimuonesha mshukiwa huyo saa chache baada ya shambulizi hilo akiwa katika eneo la msikiti katika mji wa Moabit, eneo ambalo ndipo lori hilo lilipotekwa na baadaye kuuawa dereva aliyekuwa akiliendesha.
Wakati huohuo kikosi maalumu cha polisi mjini Berlin kilivamia eneo linalodaiwa kutumiwa na wafuasi wa makundi ya itikadi kali ambalo inadaiwa kuwa mshukiwa Amri aliwahi kulitembelea.
Ama kwa upande mwingine waziri wa mambo ya ndani wa Ujerumani Thomas de Maiziere akizungumza baada ya kutembelea taasisi inayohusika na masuala ya uchunguzi nchini Ujerumani amesema alama za vidole zilizogunduliwa katika
lori na ushahidi mwingine uliokwishapatikana unaonyesha kuwa mshukiwa wa shambulizi hilo anaweza kuwa ndiye mhusika mkuu wa mipango ya shambulizi hilo la jumatatu.
Aidha taarifa zinazohusiana na mshukiwa huyo Anis Amri kuwa miongoni mwa orodha ya ujerumani tangu mwezi septemba ya watu wanaodhaniwa kuwa hatari zinazidi kuibua maswali juu ya hatua zinazochukuliwa na idara ya polisi nchini Ujerumani.
Mwandishi: Isaac Gamba/ DW/ipj/jm (dpa, Reuters, rbb)
Mhariri : Daniel Gakuba