Polisi Urusi yawakamata zaidi ya wafuasi 3,400 wa Navalny
24 Januari 2021Wanaharakati wamesema hayo siku ya Jumapili, na kuongeza kuwa watu 1,360 walikamatwa baada ya maandamano makubwa yaliyofanyika katika mji mkuu Moscow siku ya Jumamosi.
Watu wengine 523 walikamatwa katika mji wa bandari nchini humo wa St Petersburg. Kamishna wa haki za watoto nchini Urusi amesema takriban watoto 300 ni miongoni mwa wale ambao wanazuiliwa na polisi.
Mnamo Jumamosi, maelfu ya waandamanaji walijitokeza katika miji 100 nchini Urusi, ikiwa ndiyo maandamano makubwa ya hivi karibuni kushuhudiwa chini ya utawala wa Rais Vladimir Putin.
Wafuasi wa Navalny waapa kuendelea na maandamano
Soma pia: Mamlaka za Urusi zawaonya wanaotaka kuandamana
Wakati wa maandamano hayo mjini Moscow, polisi walikabiliana na waandamanaji, huku picha na video zikionyesha maafisa wa polisi wakiwapiga watu mateke.
Timu ya Navalny imeapa kuendelea na maandamano hayo makubwa ya kutaka Navalny aachiliwe huru.
Kwa mujibu wa timu ya Navalny, zaidi ya waandamanaji 40,000 walijitokeza mjini Moscow siku ya Jumamosi, lakini polisi imesema tofauti na timu ya Navalny inavyoeleza, idadi ya waliojitokeza ilikuwa ndogo.
Polisi Urusi wachunguzwa kwa kutumia nguvu kupita kiasi
Hayo yakijiri, kanda ya video ambayo imejitokeza ikionyesha afisa wa polisi akimpiga teke mwanamke katika mji wa St. Petersburg, imezusha ghadhabu mitandaoni na kushutumiwa vikali.
Kulingana na taarifa kwenye vyombo vya habari, mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 54, alipata jeraha kichwani, na bado amelazwa hospitalini akiwa hana fahamu.
Waendesha mashtaka wamesema wanachunguza kisa hicho, na vingine kubaini iwapo polisi walihusika katika vitendo vinavyokiuka haki za binadamu.
Jaribio la kumuua Navalny
Navalny mwenye umri wa miaka 44 alirejea Urusi wikiendi iliyopita kutoka Ujerumani alikokuwa akitibiwa baada ya jaribio la kuuawa kwa kuwekewa sumu aina ya Novichok.
Navalnyalikamatwa punde tu alipowasili katika uwanja wa ndege Moscow na kuhukumiwa kuwekwa kizuizini kwa siku 30, huku kesi ya haraka dhidi yakeikitarajiwa kuanza Jumatatu.
Navalny na timu yake wamepuuzilia mbali madai dhidi yao, wakiyaelezea kama njama za kisiasa zinazolenga kumnyamazisha.
Navalny amemnyooshea kidole cha lawama Rais Putin pamoja na idara ya ujasusi nchini humo FSB kuhusika kwenye kisa cha kuwekewa sumu.
Hata hivyo serikali ya Urusi imekanusha tuhuma hizo dhidi yake.
Nchi kadhaa za magharibi ikiwemo Marekani, Ufaransa, Umoja wa Ulaya pamoja na Canada, zimelaani hatua ya kukamatwa kwa Navalny pamoja na waandamanaji.
(DPAE, AFPE)