Polisi Uturuki yavamia gazeti la Upinzani
5 Machi 2016Polisi imetumia gesi ya kutoa machozi na maji ya kuwasha kuwatawanya mamia ya watu waliokuwa wameyazingira makao makuu ya gazeti hilo la Zaman mjini Istanbul ili kupinga kutekelezwa kwa agizo hilo la mahakama.
Gazeti la Zaman linahusishwa na mhubiri mwenye makao yake nchini Marekani Fethullah Gulen ambaye ni hasimu wa muda mrefu wa Rais Erdogan. Shirika la habari la serikali Anatolia limeripoti kuwa mahakama imeagiza gazeti la Zaman liwekwe chini ya usimamizi kufuatia ombi la waendesha mashitaka wa Istanbul.
Hatua hiyo inamaanisha kuwa mahakama itawateua wasimamizi wapya watakaoendesha shughuli za gazeti hilo ambao watatarajiwa kufanyia mageuzi sera za uhariri. Hakujatolewa ufafanuzi wa maamuzi hayo yaliyochukuliwa na mahakama
Zaman yadhibitiwa
Baada ya uamuzi huo wa mahakama kutangazwa, mamia ya waandamanaji walikusanyika nje ya makao makuu ya Zaman wakisubiri kuwasili kwa maafisa wa mahakama na maafisa wa usalama. Mabango yaliyobebwa na waandamanaji hao yalibeba ujumbe kuwa watapigania uhuru wa vyombo vya habari na hawatasalia kimya.
Mhariri mkuu wa gazeti hilo la upinzani Abdulhamit Bilici amenukuliwa na shirika la habari la Cihan akisema demokrasia itaendelea na uhuru wa wanahabari hautazimwa.
Bilici ameongeza kusema anaamini uandishi wa habari ulio huru utaendelea hata kama watalazimika kuandika katika kuta kwani haamini kuwa inawezekana kuvinyamazisha vyombo vya habari katika enzi hii ya mfumo wa kidijitali.
Muda mfupi kabla ya saa sita usiku, kundi la askari liliwasili katika ofisi za gazeti hilo likiwa na magari ya kumwaga maji ya kuwasha na kuutawanya umati uliokuwepo.
Askari hao waliyavamia majengo ya gazeti hilo na kuyadhibiti ili kutekeleza rasmi agizo la mahakama.
Marekani imesema agizo hilo la mahakama la kuliweka gazeti la Zaman chini ya usimamizi wa muamana ni muendelezo wa hatua zinazotia wasiwasi zinazochukuliwa na idara za mahakama na usalama kutekeleza mipango ya serikali ya Uturuki ya kuwalenga watu na mashirika ya habari yanayoikosoa.
Msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa Marekani John Kirby amesema wanawahimiza viongozi wa Uturuki kuhakikisha hatua zao zinazingatia misingi ya kimataifa ya kuheshimu demokrasia kama ilivyoelezwa katika katiba ya nchi hiyo ikiwemo kuheshimu uhuru wa kujieleza na hasa uhuru wa vyombo vya habari.
Gulen mkosaji mkubwa wa Erdogan amekuwa nchini Marekani tangu mwaka 1999 alipotoroka mashitaka dhidi yake yaliyotolewa na maafisa wa zamani wa serikali iliyopita.
Uturuki imekuwa ikiitaka Marekani kumrejesha nyumbani mhubiri huyo lakini Marekani haijaonyesha nia ya kufanya hivyo. Licha ya kuwa uhamishoni, Gulen amejijengea ushawishi mkubwa Uturuki kupitia kuwa na washirika katika idara za polisi, mahakama na kuwekeza kifedha nchini humo ikiwemo kuwa na shule chungu nzima kote Uturuki.
Wanahabari wakamatwa, vituo vyafungwa
Uturuki sasa inamshutumu Gulen kwa kuendesha kile inachokitaja kundi la kigaidi lijulikanalo Fethullahaci linalotizamwa kuwa mfumo sambamba wa serikali ambao unadaiwa kuwa na dhamira ya kuipindua serikali ya Uturuki.
Kumekuwa na misako mingi dhidi ya watu na mashirika yanayohusishwa na kundi hilo la Fethullahaci. Mnamo siku ya Ijumaa wiki hii, polisi iliwakamata wakurugenzi wakuu wanne wa mkusanyiko wa makampuni wanaoshutumiwa kumfadhili Gulen.
Chini ya utawala wa Rais Erdogan, wasiwasi umeongezeka kuwa serikali inaukandamiza uhuru wa vyombo vya habari. Serikali imekanusha madai kuwa inakandamiza uhuru wa vyombo vya habari.
Mhariri mkuu wa gazeti la Cumhuriyet Can Dundar na mhariri Erdem Gul waliachiwa huru wiki iliyopita kufuatia agizo la mahakama kuu baada ya kufungwa jela miezi mitatu kwa mashitaka ya kuchapisha siri za serikali. Hata hivyo bado wanakabiliwa na mashitaka na watafikishwa mahakamani tarehe 25 mwezi huu wa Machi.
Takriban wanahabari 2,000 wanablogu na raia wa kawaida wakiwemo wanafunzi wa shule za upili wamejikuta wakishitakiwa kwa madai ya kumtusi Rais Erdogan. Kituo huru cha televisheni cha Kikurdi IMV kilifungwa mwishoni mwa wiki iliyopita kwa shutuma za kutangaza taarifa zinazoendeleza ajenda za magaidi.
Mwandishi: Caro Robi/afp/ap
Mhariri: Yusra Buwayhid