Polisi wa Uganda wakanusha madai ya kukamatwa kwa Bobi Wine
17 Januari 2026
Polisi wa Uganda wamekanusha madai yaliyotolewa na chama cha kiongozi wa upinzani Robert Kyagulanyi maarufu Bobi Wine, kwamba kiongozi huyo alikamatwa na wanajeshi wakati Rais Yoweri Museveni akielekea kupata ushindi mkubwa katika uchaguzi wa wiki hii.
Chama cha Bobi Wine cha National Unity Platform (NUP) kilitoa taarifa jana usiku kwamba helikopta ya jeshi ilitua katika makazi yake huko Kampala na kumchukua kwa nguvu na kumpeleka sehemu isiyojulikana. Hata hivyo msemaji wa polisi wa kitaifa, Kituuma Rusoke, amedai kuwa Wine yupo nyumbani kwake na yuko huru kusafiri.
Hadi kufikia leo asubuhi, Museveni ambaye ameiongoza Uganda tangu mwaka 1986 alikuwa akiongoza kwa karibu 72% ya kura, kwa mujibu wa tume ya uchaguzi. Wine anafuatia akiwa na 24%, huku zaidi ya asilimia 90 ya vituo vya kupigia kura vikiwa tayari vimehesabiwa.