Ujerumani yaimarisha ulinzi katika Kanisa Kuu la Cologne
30 Desemba 2023Polisi wameimarisha ulinzi katika Kanisa hilo baada ya kupokea taarifa kuhusu uwezekano wa kufanyika mashambulizi ya kigaidi.
Kanisa hilo ambalo ni moja ya majengo ya kale na alama muhimu nchini Ujerumani limezuia kupokea watalaai hivi sasa. Afisa mkuu wa eneo la magharibi mwa Ujerumani Martin Lotz amesema hatua hizo za kiusalama zinalenga kuzuia shambulio lolote kama hilo bila hata hivyo kutoa maelezo zaidi. Mwanaume mmoja anashikiliwa na polisi akishukiwa kupanga shambulio dhidi ya Kanisa hilo la Cologne.
Lotz ameonya kuwa maafisa watakuwa na silaha nzito na kusema kuwa hilo ni muhimu ili kuhakikisha usalama wa raia wakati huu wa sikukuu. Hata hivyo hatua hii ya kuimarisha usalama imetokana pia na matukio ya vurugu yaliyoshuhudiwa kote Ujerumani katika mkesha wa mwaka mpya wa 2022.