1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Polisi, waandamanaji wanaopinga matokeo wapambana Msumbiji

8 Novemba 2024

Polisi nchini Msumbiji wakisaidiwa na wanajeshi walitumia mbwa na mabomu ya machozi kuwatawanya waandamanaji kwenye mji mkuu, Maputo, jana Alhamisi walioingia mitaani kupinga matokeo ya uchaguzi yanayozozaniwa.

Msumbiji| Maputo
Vikosi vya Usalama vikiwa mitaani kupambana na waandamanaji nchini Msumbiji.Picha: Amós Fernando/DW

Taifa hilo la kusini mwa Afrika limetumbukia kwenye machafuko tangu kutolewa matokeo ya uchaguzi wa rais wa Oktoba 9 yaliyompa ushindi wa asilimia 71 mgombea wa chama tawala cha Frelimo, Daniel Chapo.

Kiongozi wa upinzani Venancio Mondlane, anayesema matokeo ya uchaguzi wa rais yalikuwa ya udanganyifu na kwamba yeye ndiye mshindi, aliitisha maandamano hapo jana akisema ni muhimu kwa mustakabali wa taifa hilo.

Maelfu ya wafuasi wake waliingia mitaani kupinga matokeo hayo baadhi wakirusha mawe na kuweka vizuizi njiani kwa kuchoma matairi na mapipa ya taka. Maduka, mabenki, shule na vyuo vikuu vilifungwa mjini Maputo.

Polisi waliojihami kwa silaha na magari ya kivita waliwatawanya waandamanaji kwa kutumia mabomu na baada ya saa kadhaa hali ya utulivu ilirejea.