Polisi wafyatua mabomu ya kutoa machozi Uturuki
1 Juni 2014Maafisa walifunga njia na kuzuwia usafiri wa umma ili watu wasiweze kuingia katika uwanja wa Taksim pamoja na bustani ya karibu ya Gezi ambako serikali inapanga kupitisha matrekta katika eneo hilo lenye miti na kujenga jengo la maduka suala lililozusha vurugu mwaka jana.
Polisi walijiweka katika mstari mrefu kuwazuwia wanaharakati ambao walitarajia kusoma taarifa yao katika uwanja wa Taksim na kuweka maua katika uwanja huo katika kumbukumbu ya vifo vya kiasi watu sita katika maandamano dhidi ya utawala wa waziri mkuu Tayyip Erdogan.
Hasira dhidi ya Erdogan
Watu wengine sita wameuwawa katika machafuko yaliyotokea bila kutarajiwa katika miezi iliyofuatia wakati hasira dhidi ya Erdogan na chama chake cha AK zikitokota.
Maandamano ya mitaani huenda ni kitu kitakachojitokeza mara kwa mara katika wakati wa kuelekea uchaguzi mkuu wa rais hapo Agosti ambapo Erdogan anatarajiwa kugombea, lakini wachache wanatarajia hali hiyo kuzusha athari kubwa za kisiasa kwa kiongozi huyo ambaye ameshika wadhifa wa waziri mkuu mara tatu.
Afisa wa ngazi ya juu wa chama cha AK amesema siku ya Jumamosi kuwa Erdogan atagombea wadhifa wa urais na kuiongoza Uturuki hadi 2023.
Karibu na uwanja wa Taksim, mamia ya watu waliimba , "jiuzulu, wauwaji AKP" na "kila mahali ni Taksim, kila mahali ni upinzani" kabla ya polisi kufyatua gesi ya kutoa machozi dhidi ya kundi la watu, na kuwalazimisha kurudi nyuma.
Waandamanaji wakamatwa
Watu wanane wamekamatwa na wengine 13 wamejeruhiwa katika mapambano na polisi, chama cha kutetea haki za binadamu nchini Uturuki kimesema. Helikopta za polisi zilikuwa zikizunguka angani. Watalii ambao walikuwa na mizigo yao walilazimika kuondoka kwa haraka mahali hapo na kuepuka gesi hiyo ya kutoa machozi.
Waandamaji mia kadha waliobeba mabango yenye maandishi ya kisiasa waliwakimbia polisi katika mteremko kuelekea eneo la ujia wa maji wa Bosphorus, ujia ambao unaugawa mji wa Istanbul, mji mkubwa katika Ulaya ambao una wakaazi milioni 14.
Polisi pia walivunja maandamano katika mji mkuu Ankara na mji wa kusini wa Adana, kwa mujibu wa kituo cha utangazaji cha CNN nchini Uturuki.
Katika maeneo mengine ya mji wa Istanbul, wakaazi walifungua madirisha na kugonga mabakuli na sufuria, ikiwa ni njia ya wenyeji kuonesha kutoridhishwa kwao, hali iliyokuwa ikitumika wakati wote wa maandamano katika bustani ya Gezi.
Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre
Mhariri : Bruce Amani