1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Polisi yatumia mabomu ya kutoa machozi Cologne

10 Januari 2016

Polisi mjini Cologne ilitumia mabomu ya kutoa machozi na mabomba ya maji kulitawanya kundi la waandamanaji wafuasi wa vuguvugu linalochochea chuki dhidi ya wageni PEGIDA , na baadae maandamano hayo kugeuka ya ghasia.

Köln Pegida rechte Demonstranten
Maandamano ya kundi la PEGIDA mjini ColognePicha: Reuters/W.Rattay

Wakati hasira zikiongezeka kutokana na kiwango cha mashambulio ya kingono , waungaji mkono wa kundi hilo lenye chuki dhidi ya wageni PEGIDA waliandamana.

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel hata hivyo jana Jumamosi (09.01.2016)aliunga mkono sheria kali kuwafukuza wakimbizi wanaopatikana na hatia , katika wakati mapambano yalizuka mjini Cologne kati ya polisi na waandamanaji wa mrengo wa kulia kuhusiana na kadhia hiyo ya udhalilishaji kingono.

Maandamano katika eneo la kanisa kuu mjini ColognePicha: DW/D. Regev

Polisi yatumia mabomu ya kutoa machozi

Polisi mjini Cologne imesema imerikodi kesi 379 za udhalilishaji kingono katika sherehe za mkesha wa mwaka mpya--kuanzia kutomaswa wanawake hadi wizi pamoja na matukio mawili ya ubakaji --- ambapo watu wanaoomba hifadhi pamoja na wahamiaji kinyume na sheria wakiwa ndio wengi miongoni mwa watuhumiwa.

Polisi walitumia mabomu ya kutoa machozi na mabomba ya maji kutawanya maandamano ya waungaji mkono vuguvugu la mrengo wa kulia baada ya waandamanaji kurusha fashifashi na chupa dhidi ya maafisa wa polisi ambao wanasema walishindwa kuzuwia mashambulizi ya mkesha wa sherehe za mwaka mpya dhidi ya wanawake.

Akiahidi kuchukua hatua kali, Merkel alitangaza kwamba mkimbizi yeyote atakayepewa hukumu ya kifungo jela --- hata kama ni kifungo cha nje -- ataondolewa kutoka nchi hiyo.

Polisi wakimpambana na waandamanaji mjini ColognePicha: Reuters/I.Fassbender

Iwapo sheria haitoshelezi, basi ibadilishwe," amesema, akiahidi hatua hii haitolinda raia wa Ujerumani tu, lakini hata wakimbizi ambao hawana hatia pia.

Watu walioshuhudia wameelezea kuhusu hali ya kuogofya ya mamia ya wanawake wakilikimbia kundi la wanaume waliokuwa wakiwashika shika, matusi na uporaji katika ghasia zilizofanywa na kundi hilo.

Katika kesi zilizoripotiwa hadi sasa , asilimia 40 zinahusiana na ghasia za kingono, polisi ya mjini Cologne imesema katika taarifa.

Raia wa mataifa ya Afrika kaskazini

Madai hayo yameongeza ukosoaji wa sera za kiliberali za kansela Merkel za milango wazi -- ambazo zimesababisha kuingia kwa waombaji wapya wa hifadhi milioni 1.1 nchini Ujerumani mwaka uliopita.

"Wale wanaolengwa katika uchunguzi wa polisi wengi wao ni kutoka mataifa ya Afrika kaskazini . Wengi wao ni wanaotafuta hifadhi na watu ambao wako nchini Ujerumani kinyume na sheria," polisi imeongeza, ikithibitisha maelezo ya watu walioshuhudia.

Maandamano ya kundi la PEGIDA mjini ColognePicha: Reuters/I.Fassbender

Wakati maswali yanaongezeka juu ya uwezo wa nchi hiyo kuwajumuisha watu hao wapya, imesadifu siku ya Jumamosi kwamba mtu mmoja aliyeuwawa akijaribu kushambulia kituo cha polisi mjini Paris siku ya Alhamis aliishi akiomba hifadhi ya ukimbizi nchini Ujerumani.

Wakikiri kuwa wamevamia nyumba anakoishi mtu huyo, polisi ya Ujerumani haikufafanua iwapo alikuwa mkombizi anayeomba hifadhi, lakini chanzo karibu na suala hilo kimeliambia shirika la habari la Ufaransa AFP kwamba mtu huyo alijiandikisha kuomba hifadhi ya ukimbizi.

Mjini Cologne maelfu ya waungaji mkono wa kundi la PEGIDA walipeperusha bendera ya Ujerumani na mabango yanayosema "Wakimbizi wanaobaka hawatakiwi", wakati wakipiga makelele "Merkel raus" Merkel aondoke.

Maandamano dhidi ya unyanyasaji kingono wanawake mjini ColognePicha: Reuters/W. Rattay

Milio ya helikopta zikizunguka hewani pamoja na milio ya miripuko ya hapa na pale iliongeza hali ya wasi wasi wakati waandamanaji wanaopinga kundi la PEGIDA , wakitenganishwa na polisi , waliimba "Nazis raus" Wanazi waondoke.

Chama cha mrengo wa kulia cha Alternative for Germany, ambacho uchunguzi wa maoni unaonesha kupata asilimia 10 ya uungwaji mkono kabla ya uchaguzi mkuu wa majimbo mwaka huu, kimedai kwamba ghasia hizo zinatoa "hali ya kuporomoka kwa utamaduni na ustaarabu".

Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe

Mhariri:

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW