Polisi watumia vitoa machozi kutawanya waandamanaji Nanyuki
9 Juni 2026
Polisi nchini Kenya wametumia mabomu ya machozi kuwatawanya waandamanaji katika mji wa Nanyuki waliokuwa wakipinga ujenzi wa kituo cha karantini kwa raia wa Marekani walioambukizwa ugonjwa wa Ebola.
Karantini hiyo inajengwa katika kambi ya jeshi la anga, jambo ambalo limezua hasira miongoni mwa baadhi ya Wakenya wanaodai kuwa Marekani inahamishia hatari za kiafya zinazohusiana na mlipuko wa Ebola kutoka DRC na Uganda.
Wiki iliyopita, watu wawili walifariki katika maandamano dhidi ya mradi huo. Licha ya amri za mahakama kusitisha ujenzi, mamlaka za Kenya na Marekani zimeendelea kuunga mkono mpango huo.
Utawala wa Rais wa Marekani, Donald Trump, umesema hautaruhusu wagonjwa wa Ebola kuingia Marekani. Kituo hicho kinatarajiwa kuwahudumia Wamarekani waliowekwa chini ya uangalizi baada ya kuathiriwa na virusi lakini ambao bado hawajaonyesha dalili.
Wakati huo huo, ndege za kijeshi za Marekani zimeendelea kuwasili na vifaa pamoja na wafanyakazi wa mradi huo, huku serikali ya Marekani ikisema inaendelea kushirikiana na Kenya kutatua changamoto za kisheria zinazoukabili mpango huo.