1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Polisi wazingira makazi ya waziri wa zamani Kenya

9 Februari 2023

Makaazi ya waziri wa zamani wa usalama wa ndani nchini Kenya, Fred Matiang'i, yalizingirwa Jumatano usiku, huku kukiwa na ripoti kwamba polisi walikuwa wanapanga kumkamata kwa sababu ambazo hazikuwekwa wazi.

Kenia | Drogenhandel | Fred Matiang'i
Picha: Getty Images/AFP/S. Maina

Jumatano jioni watu waliotambuliwa kuwa maafisa wa polisi walizingira makaazi ya Matiang'i yaliyoko eneo la Karen jijini Nairobi kabla ya saa nne usiku na walikuwa wanajaribu kulazimisha kuingia ndani.

Kiongozi wa muungano wa upinzani wa Azimio la Umoja, Raila Odinga, aliwasili nyumbani kwa Matiang'i majira ya saa nne usiku huo, akitaka kubaini sababu za polisi hao kuzingira makaazi ya waziri huyo wa zamani.

Timu ya wanasheria wa Matiang'i ambao pia walikuwepo nyumbani hapo, walielezea hatua hiyo kuwa ya kinyume na utaratibu na kudai maisha yake huenda yakawa hatarini.

Soma pia: Mahakama Kenya yawapiga faini waziri, mkuu wa polisi

Odinga: 'Tunarudi enzi za giza'

Bwana Odinga aliikosoa serikali ya Rais William Ruto, akisema hivyo sivyo anavyopaswa kutendewa waziri wa zamani wa usalama wa ndani.

"Hivi sasa tunashuhudia kile ambacho nchi hii imepitia hapo kabla, nyakati za ukamataji wa usiku wa manane na kuzuwiliwa watu bila mashtaka yoyote," alisema Odinga.

Kiongozi wa muungano wa upinzani wa Azimio la Umoja , One Kenya, Raila Odinga, ameukosoa utawala wa Rais William Ruto kwa kuwandama mawaziri wa zamani.Picha: Thomas Mukoya/REUTERS

Odinga alisema ikiwa bwana Matiang'i alitenda kosa, ni Mkenya na anaishi Kenya, kuna muda wa kumpatia wito wa kuripoti kituo cha polisi.

Ripoti za awali zilisema Tume ya Maadili na Kuzuwia Rushwa ndiyo iliyokuwa inamfuatilia Matiang'i, lakini mkuu wa tume hiyo, Twalib Mbarak, alisema kwamba timu yake haihusiki kwa vyovyote na uvamizi huo.

Soma pia: Kenya: Polisi ahukumiwa kifo kwa kumuua wakili Willie Kimani

Chanzo kimoja kilichokuwepo kwenye eneo la tukio kilifahamisha kwamba Matiang'i alikuwa amearifiwa kuhusu ukaguzi ambao ungefanyika nyumbani kwake, lakini polisi walionekana kurudi nyuma baada ya kuwasili kwa mawakili na watu wengine.

Polisi yakanusha maafisa wake kuhusika

Hata hivyo, mkuu wa jeshi la polisi nchini humo, Japhet Koome, katika mazungumzo na gazeti la Nation, amesema hakuna afisa wa polisi anayehudumu chini ya jeshi hilo aliyetumwa kwenda nyumbani kwa Matiang'i. 

Lakini wakili wa Matiang'i, Dunstan Omari, amepinga kauli hiyo ya Koome, akihoji kwa nini polisi haikupeleka maafisa wake kuchunguza uvamizi huo ikiwa wavamizi hawakuwa maafisa wa polisi.

Mkuu wa jeshi la Polisu Japhet Koome amesema hakuna afisa wa jeshi alietumwa kwenda kwa Matiang'i.Picha: Yasuyoshi Chiba/AFP

Omari amesema inaonekana kuna mpango wa makusudi wa kuwalenga mawaziri wa zamani, na kuongeza kuwa wanatafuta muongozo wa kuwawekea dhamana tangulizi.

Matiang'i amekimbilia mahakamani akiutaka mhimili huo kutoa amri ya kuizuwia polisi kumkamata kiholela, kumshtaki, kumnyanyasa au kuingilia mambo yake pasina kufanya uchunguzi, kwa kulingana naye, kupata fursa ya kusikilizwa kwa kupewa samansi kufika ofisi zozote kurekodi taarifa ikiwa itahitajika.

Chanzo: Mashirika

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW