1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vijana Kenya waonywa kutoandamana kufika uwanja wa ndege

23 Julai 2024

Polisi nchini Kenya imewataka waandamanaji kuepuka kuandamana kuelekea uwanja wa kimataifa wa Jomo Kenyatta na maeneo yaliyo karibu na uwanja huo.

Maandamano ya kuipinga serikali yafanyika mjini Nairobi
Polisi ya Kenya imeonya dhidi ya maandamano katika eneo la uwanja wa ndege wa Jomo Kenyatta mjini NairobiPicha: Luis Tato/AFP

Mamlaka ya uwanja wa ndege ya Kenya imewashauri abiria wanaotumia uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta kufika mapema kuliko kawaida. Tahadhari hiyo inatokana na hatua ya baadhi ya waandamanaji kujipanga kukusanyika katika maeneo ya uwanja huo.

Kaimu Inspekta Jenerali wa polisi nchini humo Douglas Kanja Kirocho amewaonya waandamanaji dhidi ya jaribio hilo la kuuvamia uwanja wa ndege akisema polisi ina ripoti za kijasusi zinazoonyesha maandamano ya sasa yametekwa nyara na wahalifu.

Katika siku chache zilizopita polisi ilisema maandamano, ambayo yamegharimu maisha ya watu karibu 50 tangu kuripuka kwake mwezi mmoja uliopita yameingiliwa na magenge ya wahalifu.

Ruto asema maandamano Kenya lazima yakomeshwe, upinzani wahimiza 'haki'

Vijana wataandamana hadi rais Ruto atakapoondoka madarakani.

Waandamanaji wanaendelea na maandamano licha ya onyo kutoka kwa polisi dhidi ya kuendelea na maandamano yao. Picha: Monicah Mwangi/REUTERS

Vijana wamekuwa wakiongoza maandamano nchini Kenya wakipinga hatua ya serikali kuongeza ushuru, licha ya rais William Ruto kuondoa muswada wa fedha uliokuwa na utata wa 2024/2025 na kulifuta karibu baraza lake lote la mawaziri. Ruto baadae aliwarejesha kazini baadhi ya mawaziri katika baraza hilo wiki iliyopita. 

Wachambuzi wanasema vijana wameapa kuendelea na maandamano yao hadi pale rais Ruto atakapoondoka madarakani. Vijana pia wanataka pia mageuzi katika kupambana na ufisadi, wanataka utawala bora na utoaji wa huduma zilizobora zaidi katika serikali za kaunti na serikali kuu. 

Awali maandamano yaliingiliwa na watu waliodaiwa kuwa wahalifu kwa nia ya kuzua vurugu na kupoteza dira ya waandamanaji vijana maarufu kama Gen Z, wanaotaka mabadiliko katika mfumo wa uongozi katika taifa hilo la Afrika Mashariki. 

Rais wa Kenya amerejea sehemu kubwa ya mawaziri wa zamani

Maandamano ya leo tayari yameshuhudiwa mjini Nairobi, Kisumu na katika baadhi ya maeneo mjini Mombasa na maeneo mengine ya nchi. 
 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW