1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Polisi ya Kenya yashutumiwa kwa ukatili

22 Aprili 2020

Shirika la kimataifa la kutetea haki za Binadamu la Human Rights Watch (HRW), limeishutumu polisi ya Kenya kwa kuwaua watu 6 na kuwapiga wengine kadhaa kando na kuwapora, wakati wa kutekeleza amri ya kutotoka nje usiku.

Kenia Drei Tote bei Überfall auf Bus
Picha: Reuters/Str

Amri hiyo ya kutotoka nje usiku inaanzia saa moja usiku hadi saa kumi na moja alfajiri, ili kuzuia kusambaa kwa virusi vya corona. Amri hiyo ilitangazwa Machi 27.

Shirika hilo la HRW limesema tokea mwanzo, maafisa wa polisi walitekeleza amri hiyo kwa njia ya fujo, wakati mwingine wakiwapiga watu kwa viboko, mateke na kuwafyatulia gesi za kutoa machozi kuwalazimisha kuondoka barabarani au mitaani. HRW imeongeza kuwa watu sita waliuawa wakati wa purukushani hizo.

Shirika hilo limeeleza kuhusu kisa cha mvulana mwenye umri wa miaka 13 aliyeuawa mjini Nairobi mnamo Machi 31 baada ya kupigwa risasi akiwa amesimama kwenye baraza la nyumba yao, wakati polisi walipokuwa wakiwalazimisha watu kuingia majumbani.

Katika kisa kingine, mwanamke muuza nyanya mjini Kakamega, magharibi mwa nchi hiyo, alifariki baada ya kupigwa na mtungi wa gesi ya kutoa machozi.

Wanaume walipigwa na polisi hadi wakafariki

Wanaume wengine wanne walipigwa na polisi hadi kufa katika maeneo tofauti tofauti ya nchi.

Kwenye taarifa ambayo shirika hilo limetoa siku ya Jumanne, afisa wake mkuu wa utafiti barani Afrika Dr. Otsieno Namwaya amesema inashtusha kuwa watu wanauawa na kupoteza maisha yao ya kila siku, wakati wanapopaswa kulindwa dhidi ya maambukizi ya virusi vya corona.

Polisi wakiwa wamewalaza chini raia huko Mombasa pwani ya KenyaPicha: picture-alliance/AP Photo

"Polisi kutumia nguvu kupita kiasi, si kinyume tu cha sheria bali pia hakuleti tija katika vita dhidi ya kusambaa kwa virusi vya corona." Alisema Dr. Otsieno.

Shirika hilo limewahimiza maafisa kufanya uchunguzi wa dharura kuhusu visa vya dhuluma za polisi.

Mara kwa mara, mashirika ya kutetea haki za binadamu huishutumu polisi ya Kenya kwa kutumia nguvu nyingi na kufanya mauaji ya kiholela hususan katika mitaa ya watu maskini.

Mnamo mwezi Januari, shirika la HRW lilisema kuwa tangu sikukuu ya Krismasi iliyopita, watu wanane walipigwa risasi katika mitaa mitatu ya watu maskini. Ripoti ya mwaka 2019, nayo iliainisha vifo vya vijana 21 waliouawa na polisi bila sababu maalumu.

Rais Uhuru Kenyatta aliwaomba radhi Wakenya kwa ukatili wa polisi

Taarifa ya HRW imeeleza kuwa japo visa vingi vya mauaji yanayofanywa na polisi pamoja na matumizi ya nguvu kupita kiasi vimeripotiwa na mashirika mbalimbali yakiwemo mashirika ya serikali na ya kutetea haki za binadamu, lakini ni nadra sana kwa maafisa hao kuwajibishwa.

Mnamo Aprili 1, rais wa Kenya Uhuru Kenyatta, aliomba radhi, kutokana na polisi kutumia nguvu kupitiliza wakati wa kutekeleza amri ya kutotoka nje.

Maafisa wanaokabiliana na virusi vya corona Kenya wakiwa kaziniPicha: Reuters/B. Ratner

Shirika la HRW lilimkosoa Rais Kenyatta kwa kutotoa amri ya kusitishwa kwa dhuluma hizo za polisi.

Msemaji wa polisi Charles Owino, alikiri kuwepo kwa baadhi ya matatizo, lakini aliongeza kuwa yalishasuluhishwa.

"Tuna mikakati ya kuwashughulikia polisi wanaopotoka, na kwa kweli tulikuwa na shida siku ya kwanza ya kutekeleza amri ya kutokuwa nje usiku, na hizo kesi zimeshashughulikiwa." Owino aliliambia shirika la habari la AFP na kuongeza kuwa kile shirika la HRW linafanya ni ukiukaji wa demokrasia. "Wanapaswa kutumia fedha kuwahimiza watu kufuata sheria badsla ya kuishutumu polisi." Akaongezea.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW