1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Polisi ya Tanzania yazuia maandamano ya CHADEMA

13 Septemba 2024

Jeshi la polisi nchini Tanzania limezuia maandamano yaliyopangwa kufanywa na chama kikuu cha upinzani nchini humo, CHADEMA Septemba 23 likisema maandamano hayo ni kielelezo cha uvunjifu wa amani.

Mwenyekiti wa CHADEMA Freeman Mbowe
Jeshi la polisi nchini Tanzania limekizuia chama cha upinzani nchini Tanzania kuandamana Septemba 23, 2024Picha: Ericky Boniphace/DW

CHADEMA aidha, imeipa serikali hadi tarehe 21 mwezi huu kuhakikisha kuwa viongozi na wanachama wake kinaodai wametekwa na kupotezwa wawe wamepatikana au vyenginevyo watachukua hatua. 

Zuio hili linatolewa siku chache baada ya CHADEMA kutangaza kuwa kitafanya maandamano nchi nzima Septemba 23 ili kuishinikiza serikali kueleza hatua iliyofikiwa kuhusu matukio ya watu kutekwa na kuuawa.

Soma pia:Chadema: Maandamano yatafanyika kama yalivyopagwa

Leo, akiwa mkoani Kilimanjaro, Msemaji Mkuu wa Jeshi la Polisi, David Misime, amewapa onyo viongozi wa CHADEMA kuacha kuwahamasisha wananchi kushiriki maandamano hayo.

"Jeshi la polisi linatoa onyo kwa viongozi kuacha kuwahamasisha wafuasi wa chama hicho kujihusisha katika uhalifu huo, na yoyote atakayeingia barabarani atakabiliwa vilivyo kwa mujibu wa sheria ya nchi."

Viongozi na wafuasi wa CHADEMA wameonywa kuhusu kuandamana Septemba 23, 2024 Picha: Eric Boniface/DW

Kadhalika Kamanda Misime amesema maandamano hayo ni haramu na akaapa kuwa hayatafanyika. Hivyo akawashauri wale walioalikwa na CHADEMA kutoka mikoani kufika Dar es Salaam kwa minajili ya kuandamana, wasikubali kurubuniwa au kushawishiwa kushiriki katika maandamano hayo.

Septemba 11, CHADEMA katika mkutano wake na vyombo vya habari, walitangaza azma yao ya kufanya maandamano nchi nzima ili kushiriki maandamano, kuishiniza serikali kuchukua hatua baada ya mfululizo wa matukio ya watu kutekwa na kuuawa.

Soma zaidi: Chadema yaikosoa serikali baada ya kuteswa kwa viongozi wake

Akizungumza na DW, mara baada ya kauli hiyo kutoka kwa Jeshi la Polisi, Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uchechemuzi wa chama hicho John Mrema alielezwa kushangazwa na hatua hii ya jeshi la polisi na kuhoji maandamano yanawezaje kuvuruga uchaguzi unaofanywa na jeshi hilo.

"Hatuandamani kwenda vituo vya polisi wala makao makuu ya jeshi la polisi. Wao waendelee na uchunguzi lakini sisi tulisema kama watu wetu hawatapatikana wakiwa hai ama wamekufa basi tutaanza kuwadai kwa sababu tumechoka," aliongeza Mrema.

Septemba 8, Rais Samia Suluhu Hassan aliviagiza vyombo vya usalama kufanya uchunguzi wa kifo cha kada wa CHADEMA, Ali Kibao aliyekutwa ameuawaPicha: Presidential Press Service Tanzania

Septemba 8, mara baada ya taarifa za kutekwa na kuuawa kwa kada wa CHADEMA, Ali Kibao, Rais Samia Suluhu Hassan kupitia mtandao wake wa X aliagiza vyombo vya usalama kufanya uchunguzi wa kina na kumpelekea taarifa.

Alhamisi hii, Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania, IGP, Camillius Wambura, akizungumza katika ufunguzi wa Mkutano wa Mwaka wa Maafisa Wakuu Waandamizi wa Jeshi la Polisi mkoani Kilimanjaro alisema hali ya nchi ni shwari.

Hivi karibuni, kada wa CHADEMA na mjumbe wa Sekretarieti ya chama hicho, Ali Kibao, alitekwa akiwa katika basi na baadaye kukutwa akiwa amefariki maeneo ya Ununio, Tegeta, jijini hapa.

Sambamba na hilo, baadhi ya viongozi wa CHADEMA, akiwamo Katibu wa Jimbo la Temeke, Jacob Mlay, Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la CHADEMA (BAVICHA), Wilaya ya Temeke, Deusdedith Soka na Dereva wa pikipiki ya kubeba abiria, Frank Mbise, mpaka sasa hawajulikani walipo.