Polisi yakabiliana na waandamanaji Uturuki
15 Mei 2014Mripuko uliotokea usiku wa jana umezua ghadhabu kote Uturuki, ambapo vyama vinne vikuu vya wafanyakazi vimetengaza mgomo wa kitaifa wa siku moja kuishinikiza serikali kuweka mazingira mazuri ya kazi kwa wachimba madini.
Katika mji wa magharibi wa Izmir, ulio umbali wa kilomita 60 kutoka palipotokea ajali hiyo, polisi wametumia magari ya maji yanayowasha na mabomu ya machozi kuvunja maandamano ya watu wapatao 20,000.
Katika mji mkuu, Ankara, polisi walitumia njia kama hizo kulichawanya kundi dogo la waandamanaji wapatao 200, ikiwa ni siku moja baada ya maelfu kuandamana. Hali kama hiyo imeripotiwa mjini Istanbul.
Waandamanaji wanailaumu serikali ya Waziri Mkuu Tayyip Erdogan kwa uzembe. Abdulghafar Karakoc ni mchimba madini mstaafu ambaye ameliambia shirika la habari la Reuters kwamba tamaa ya wamiliki migodi ndiyo inayowaponza wachimbaji:
"Wanawashinikiza wachimba madini kupata makaa ya mawe mengi zaidi. Kwao wao, hilo ndilo wanalojali tu. Hawajali wale wanaokufa. Moto huchoma unapotua, lakini kampuni zinataka makaa ya mawe tu, na sio matatizo ya wafanyakazi."
Msiba wa kitaifa, asema Rais Gul
Leo Rais Abdullah Gul amelitembelea eneo hilo na kusema kwamba msiba huo ni mkubwa sana kwa Uturuki na kwamba serikali itafanya kila iwezalo kuwaokoa waliokwama.
"Maumivu yetu ni makubwa mno. Maumivu haya si ya watu wa hapa Soma tu, bali kwa taifa zima la Uturuki. Tunakabiliwa na maafa makubwa." Amesema Rais Gul.
Kwengineko, mazishi ya wahanga wa ajali hiyo mbaya kabisa kwenye sekta ya madini nchini Uturuki, wameendelea kuzikwa, huku ndugu na jamaa wakielezea masikitiko yao.
Mazishi yafanyika
Katika mji wa Misana, waandishi wa habari wameshuhudia safu za makaburi yaliyowazi yakisubiri kupokea maiti. Mmoja wa waliopoteza watoto wao, Bi Sefer Hazar, amesema sasa kilichobakia ni huzuni.
"Alikuwa na watoto wawili. Mke wake amefadhaika. Familia yetu nzima imefadhaika. Si pekee, tuna jamaa wengine waliokufa pia. Watazikwa hapa leo. Ndio hivi tunawasubiri," amesema bibi huyo.
Hadi sasa ni watu 282 waliothibitishwa kupoteza maisha yao, huku muendeshaji wa mgodi huo, Soma Komur Isletmeleri, akisema waliookolewa ni wachimbaji 450 na kwamba waliokufa ni wale waliovuta hewa ya sumu.
Lakini tangu alfajiri ya jana, hakuna mchimba madini hata mmoja aliyetolewa akiwa hai, hali inayoashiria kuwa wengine zaidi ya 100 waliobakia ndani, umbali wa kilomita mbili chini ya ardhi, wana nafasi ndogo sana ya kupatikana wakiwa hai.
Hata hivyo, bado waokoaji wanajaribu kuzifikia sehemu walipokwama wachimbaji hao, ikiwa ni masaa 48 tangu moto kuharibu kabisa mfumo wa umeme kwenye mgodi huo na, hivyo, kuwafanya wafanyakazi waliokwama chini ya ardhi kushindwa kutumia lifti kujiokoa.
Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters/dpa
Mhariri: Josephat Charo