1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Polisi yaonya upinzani kuhusu maandamano Kenya

Shisia Wasilwa
1 Mei 2023

Jeshi la polisi limewaonya viongozi wa Muungano wa Azimio dhidi ya kufanya maandamano siku ya Jumanne, baada ya Rais William Ruto kuapa kwamba hatakubali tena kuacha wimbi la maandamano kuendelea.

Jeshi la polisi nchini Kenya limewanya viongozi wa Muungano wa Azimio dhidi ya kufanya maandamano
Jeshi la polisi nchini Kenya limewanya viongozi wa Muungano wa Azimio dhidi ya kufanya maandamanoPicha: Yasuyoshi Chiba/AFP

Kwenye kikao na wanahabari, Kamanda Mkuu wa Polisi jijini Nairobi nchini Kenya, Adamson Bungei, amesema hata kama muungano wa Azimio ulishaomba ruhusa ya kufanya maandamano, lakini katiba haijatoa haki hiyo kwa ukamilifu. Kwa msingi huo, kamanda huyo mkuu wa polisi amepiga marufuku maanadamano hayo akidai kuwa katika matukio ya nyuma waandamanaji wa Azimio walishiriki kwenye ghasia, kuharibu mali huku watu wasio na hatia wakishambuliwa na hivyo kusababisha maafa.

"Tunakataa kuruhusu maandamano ya muungano wa Azimio kwenye barua hii. Maandamano yoyote yatakabiliwa na maafisa wa kudumisha sheria.”, alisema Bungei.

Haki za kikatiba

Katiba ya Kenya kwenye kifungu chake cha 5a kinaelezea utaratibu wa kufanyika mikutano na maandamano, ambapo jeshi la polisi linastahili kufahamishwa juu ya kufanyika kwake, ingawa pia lina mamlaka ya kukubali ama kukataa kutoa kibali cha maandamano hayo kulingana na mazingira.

Taarifa ya Bungei inajiri pia siku chache baada ya Rais William Ruto kuwaonya viongozi wa Azimio dhidi ya kufanya maandamano, huku mazungumzo ya mapatano kati yao na serikali yakiendelea.

"Mimi ni commander in chief, nyinyi mtajua hamjui...hakuna mali ya wananchi itaharibika tena, hakuna biashara ya Mkenya itaharibika tena."

''Tutarudi uwanjani''

Kiongozi wa upinzani, Raila Odinga, aapa kuendelea na maandamano ya ummaPicha: Boniface Muthoni/Zuma/IMAGO

Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari, Raila Odinga amesema kuwa atawasilisha maombi yake kwenye afisi nne za serikali siku ya Jumanne. Taarifa hiyo inaendelea kusema kuwa, Raila hataketi kitako na kuangalia taifa likisambaratika. Aidha ameongeza kusema kuwa upinzani hautanyamazishwa.

"Bwana Ruto na wenzake wamekataa kutii taratibu tulizokubaliana nao. Tunarudi uwanjani.”

Waziri mkuu huyo wa zamani amesema watawasilisha maombi yao kwenye afisi za Tume ya Kusimamia Uchaguzi na Mipaka, IEBC, kuonesha kuwa matokeo ya uchaguzi mkuu yalichakachuliwa.

Kwenye maombi hayo Azimio inataka seva za IEBC zifunguliwe. Maombi mengine yatawasilishwa kwenye afisi ya Rais, kuonesha kupanda kwa gharama ya maisha huku wakimtaka Rais kukoma kuvunja vyama.

Raila amesema pia maombi mengine yatawasilishwa kwenye Wizara ya Hazina ya Taifa, kuwataka wafanyakazi wa umma wapate mishahara yao kwa wakati unaofaa na fedha kutolewa kwa majimbo haraka iwezekanavyo.

Raila amesisitiza kuwa hawatatishwa wala kutetereka kwenye azma yao. Maandamano hayo yanajiri huku uchumi wa taifa ukisuasua.