1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Polisi yatawanya waandamanaji, DRC

Sekione Kitojo
21 Januari 2018

Takribani watu watatu wameuawa wakati majeshi ya usalama yalipofyatua mabomu ya kutoa machozi na risasi kuwatawanya waandamanji wanaompinga rais Joseph Kabila, katika maandamano yaliyoandaliwa na Kanisa Katoliki.

Proteste im Kongo
Maandamano mjini KinshasaPicha: Reuters/K. Katombe

Mwandishi habari  wa  shirika  la  habari  la  Reuters alishuhudia  polisi  na  majeshi  ya  ulinzi yakifyatua  risasi  na  mabomu  ya  kutoa  machozi  hewani  nje  ya  kanisa  kuu  la  mjini Kinshasa Notre Dame. Kiasi  watu sita wamejeruhiwa  kidogo wakati  walipopigwa  na makopo ya mabomu  ya  kutoa  machozi  yaliyokuwa  yakiruka  huku  na  kule. Maandamano hayo yaliandaliwa na kanisa Katoliki.

Polisi walifyatua mabomu ya kutoa machozi mjini Kinshasa dhidi ya waandamanaji Picha: Getty Images/AFP/J. Wessels

Hasira zimekuwa zikiongezeka  dhidi  ya  Kabila tangu  pale  alipokataa  kujiondoa madarakani  mwishoni  mwa  muhula  wake kisheria Desemba 2016, na  kuzusha maandamano  mitaani  ambapo watu  kadhaa  waliuwawa  mjini  Kinshasa,  na  kusababisha kuwapo  kwa  makundi  kadhaa  ya  waasi  katika  maeneo  mengine  ya  nchi  hiyo.

Hali  hii  imeongeza  hofu  kwamba , taifa  hilo  kubwa  lenye  utajiri  mkubwa  wa  madini huenda  likarejea  tena  katika  vita  ambavyo  vimewauwa  mamilioni  ya  watu  katika  miaka ya  1990, wengi  wao  kutokana  na  njaa  na  magonjwa.

"Nimeandamana  leo kwa sababu tu: Nataka  kuwalea  watoto  wangu  katika  nchi  ambayo inaheshimu haki  za  binadamu," muandamanaji Pascal Kabeya , mwenye  umri  wa  miaka 40  mchuuzi  katika  soko , aliliambia  shirika  la  habari  la  Reuters mahali  ambapo  mamia kadhaa  ya  watu  walijikusanya   katika  kitongoji  cha  mjini  Kinshasa.

Waandamanaji wakibeba mabango ya kumpinga rais Kabila mjini KinshasaPicha: Getty Images/AFP/J. Kannah

Kanisa Katoliki

Georges Kapiamba , rais wa  chama  kinachotoa usaidizi  wa  Kisheria  nchini  Congo, Congolese Association for Access to Justice (ACAJ)kimesema idadi  ya  watu  waliouwawa kuwa  ni  watatu  na wengine 17  wamejeruhiwa. Msemaji  wa  polisi hakuweza  kupatikana mara  moja  kwa  ajili  ya  kutoa  maelezo.

Ghasia zimekuwa  kama  zile  za  mkesha  wa  mwaka  mpya, wakati majeshi  ya  Congo yalipowauwa watu saba  katika  mji  mkuu wakati  wa  maandamano  ya  wanaharakati  wa Kikatoliki.

Katika  makubaliano  baina ya  kanisa Katoliki  na  wapinzani  wa   Kabila, rais alitakiwa kujiuzulu  mwishoni  mwa  mwaka  jana, akisafisha  njia  kwa  ajili  ya  uchaguzi  uliotarajiwa kufanyika  mapema  mwaka  huu. Lakini  alikaidi makubaliano  hayo  na  uchaguzi  umekuwa ukicheleweshwa  mara  kwa  mara , na  sasa unatarajiwa  bila uhakika  kufanyika  mwishoni mwa  mwaka  huu  2018.

Rais Joseph KabilaPicha: picture-alliance/dpa/M. Kappeler

Kanisa Katoliki  limejitokeza  tangu  wakati  huo  kuwakumbatia  wapinzani  wa  juhudi  za Kabila  kuendelea  kubaki  madarakani  bila  kuwa  na  uhalali  huo, wakati  upinzani  wa kisiasa  ukiwa  bado  dhaifu  na  umegawanyika.

Kabila , ambaye  amekuwa  rais  baada  ya  baba  yake  kuuwawa  mwaka  2001, anatupa lawama  za  ucheleweshaji  huo  wa  uchaguzi  kwa  utaratibu  wa  uandikishaji  wa  wapiga kura.

Mwandishi: Sekione  Kitojo / rtre

Mhariri: Isaac Gamba