Polisi yavunja mtandao wa picha za ngono unaotumia watoto
3 Mei 2021Polisi ya ujerumani imegundua moja ya jukwaa la tovuti kubwa duniani ya chini kwa chini inayohusika na picha za ngono za watoto. Jukwaa hilo linafuatiliwa na zaidi ya watu 400,000.
Watu wanne wamakamtwa kuhusiana na jukwaa hilo kwa mujibu wa waendesha mashtaka waliotoa taarifa hiyo leo Jumatatu. Jukwaa hilo la mtandao linaloitwa ''BOYSTOWN''linafanya kazi kuanzia alau Juni mwaka 2019 kwa mujibu wa ofisi ya mwendesha mashtaka wa serikali mjini Frankfurt na polisi ya shirikisho ya kupambana na uhalifu BKA,na lilikuwa linatumika kupitia tu kile kinachoitwa Darknet,ambao ni mtandao wa siri usijulikana.
Tovuti hiyo inawafuatiliaji 400,000 na ilikuwa inatumika katika ubadilishanaji dunia nzima wa matukio ya watoto wanaofanyishwa ngono. Mtandao huo ilikuwa ukiwawezesha wanachama wake kupata matukio ya ngono za watoto na kubadilishana mikanda ya vidio kupitia sehemu ya kuandikiana ujumbe pamoja na sauti.
Waendesha mashtaka wameeleza kwamba miongoni mwa picha na rekodi za vidio zinaonesha pia matukio ya unyanyasaji mkubwa wa kingono unaofanyiwa watoto wadogo.
Kufuatia msako mkubwa uliofanywa dhidi ya majengo saba ya Ujerumani katikati ya Aprili,polisi imewakamata watu watatu wanaoshukiwa kuwa vinara wanaotuhumiwa kuendesha na kuushughulikia mtandao huo.
Washukiwa hao ni pamoja na mwanamme mmoja mwenye umri wa miaka 40 anayeishi Paderborn,huko Magharibi mwa Ujerumani na miwngine ana umri wa miaka 49 kutoka Munich wakati wa tatu ni mwanamme pia ana umri wa miaka 58 kutoka kaskazini mwa Ujerumani ambaye amekuwa akiishi Amerika ya Kusini kwa miaka mingi kwa mujibu wa polisi.
Lakini pia yuko mtu wa nne aliyekamatwa ambaye ni mwanamme mwenye umri wa miaka 64 kutoka mji wa Hamburg akishukiwa kuwa amejisajili kama mwanachama wa jukwaa hilo la mtandao mnamo Julai mwaka 2019 na alichapisha mchango wake zaidi ya 3,500 kwenye mtandao huo na kumfanya kuwa mmoja wa watumiaji wakubwa wa mtandao huo.
Msako mkubwa ulifanyika katika majimbo matatu ya Ujerumani ya North
Rhine-Westphalia, Bavaria na Hamburg.
Mwandishi Saumu Mwasimba
Mhariri.Iddi Ssessanga