1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Polisi yazingira makaazi ya Ne Mwanda Nsemi jijini Kinshasa

Saleh Mwanamilongo
24 Aprili 2020

Kiongozi huyo wa kidini Ne Mwanda Nsemi amejihami na wafuasi wake wapatao 300 na amekaidi amri ya polisi yakujisalimisha,baada vifo vya watu 14 wakiwemo polisi 2.

Polisi mjini Kinshasa wazingira makaazi ya Ne Mwanda Nsemi
Polisi mjini Kinshasa wazingira makaazi ya Ne Mwanda Nsemi Picha: Getty Images/AFP/J. Wessels

Polisi wamezingira makazi ya mbunge wa zamani na kiongozi wa kanisa jijini Kinshasa, Ne Mwanda Nsemi, wakimtaka ajisalimishe. Nsemi amejihami na wafuasi wake wapatao 300 na amekaidi amri ya polisi. Hatua hiyo imefuatia vifo vya watu 14 wakiwemo polisi 2, ambavyo vilisababishwa Jumatano na wafuasi wa kiongozi huyo wa kidini.

Mkuu wa polisi jenerali Sylvano Kasongo amesema kwamba polisi wamesubiri amri ya kumkamata kwa Ne Mwanda Nsemi baada ya kuyazingira toka jana makazi yake yanayopatikana kwenye mitaa ya kifahari ya Macampagne, kusini mwa jiji la Kinshasa.

Juhudi za kumtaka Ne Mwanda Nsemi ajisalimishe na wafuasi wake waliojihami hadi sasa hazijafua dafu. Mamia ya polisi wameonekana wakizuiwiya barabara zote zinazoelekea kwenye makazi ya Nsemi. Mashahidi wanaelezea kwamba toka jana wakaazi wengine wa maeneo hayo hawaruhusiwi kutoka nje.

Gavana na baadhi ya wasiasa wa jimbo la Kono-Central, alikotokea Nsemi walijaribu usiku kucha bila kufanikiwa kumshawishi  ili ajisalimishe kwa polisi. Hofu za kutokea vurugu katikati ya mji zimetolewa na raia wa mtaa anakoishi Ne Mwanda Nsemi endapo polisi itatumia nguvu kumtia mbaroni, kwa sababu amejihami na wanamgambo wake wanaoitwa ''makesa'' inayomanisha ''wapiganaji''.

 Serikali yatakiwa kuwajibika

Polisi wakipiga doria jijini Kinshasa ,mji mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya KongoPicha: picture alliance/AP/J. Bompengo

Mratibu wa mashirika ya kiraia mjini Kinshasa, Dieudonne Mushagalusa, amesema ni lazima serikali izingatie usalama wa raia wanaoishi kando ya makaazi ya Nsemi ikiwa polisi itatumia nguvu.

''Tunaomba serikali kuendesha uchunguzi ilikufahamu wahusika wa machafuko yaliosababisha vifo vya watu hao 14,pili serikali izingatie kwamba polisi hawatumii kunguvu ya kuzidi kiasi na tatu serikali inatakiwa kuwajibika katika ahadi zake kwa huyo Ne Mwanda Nsemi ikiwa kuna makubaliano ya aina yeyote na kiongozi huyo''.

Mbunge wa zamani na kiongozi wa Kanisa la Bundu Dia Mayala, ambaye pia anajiita kuwa ni nabii wa Mungu, Ne Muanda Nsemi, alijitokeza hadharani baada ya kuwa mafichoni kwa miaka miwili alipotoroka jela baada ya kukamatwa na polisi mwaka 2017.

Ne Mwanda Nsemi alikamatwa kwa madai ya kumkashifu  rais wa wakati huo Joseph Kabila kufuatia mwito alioutowa wa kutoheshimu taasisi zote za kitaifa. Mwezi Januari Ne Mwanda Nsemi alirejelea madai yake dhidi ya rais wa sasa Felix Tshisekedi, na kujitangaza mwenyewe kuwa rais wa Congo. Wafuasi wake walijaribu kuandamana hadi ikulu jijini Kinshasa wiki tatu zilizopita, kabla ya kukabiliana na polisi. Nsemi ametuhumiwa pia kuhusika na uchochezi wa chuki za kikabila ambazo zilisababisha wafuasi wake kuwalenga watu ambao sio wazawa wa jimbo la Kongo-Central ambao wanaishi huko.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW