1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Pompeo aanza ziara ya Afrika nchini Senegal

Yusra Buwayhid
17 Februari 2020

Akiwa nchini Senegal wakati wa ziara yake ya mataifa matatu ya Afrika Magharibi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Mike Pompeo amesema nchi yake itashirikiana na Afrika kupambana na ugaidi.

USA Washington | PK Mike Pompeo Steve Mnuchin
Picha: picture-alliance/newscom/M. Theiler

 Pompeo amesema serikali ya Rais Donald Trump inajaribu kutathmini idadi ya wanajeshi wa Marekani inayohitajika Afrika Magharibi kupambana na vurugu za makundi yenye misimamo mikali ya kidini katika eneo hilo. Pompeo ameongeza kwamba Marekani itashirikiana na Senegal na mataifa mengine ya Afrika Magharibi pamoja na Ufaransa kupambana na kitisho kinachotokana na vurugu za makundi ya kigaidi.

Waziri huyo wa Marekani alihitimisha ziara yake nchini humo hapo jana, Jumapili, kwa mkutano wa pamoja na waandishi habari akiwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Senegal, Amadou Ba. Pompeo amesema Marekani inaitegemea Senegal kushirikiana nayo kupambana na ugaidi wa misimamo mikali ya Kiislam, na kwamba itaendelea kutoa mafunzo kwa askari wa kulinda amani nchini Seenegal.

"Nimezungumza na viongozi wa Senegal kuhusu ugaidi wa makundi yenye misimamo mikali ya Kiislam, ambao unahatarisha maisha ya watu milioni 350 hapa hapa Afrika Magharibi. Unahatarisha pia maisha ya Wamarekani. Tunaitegemea Senegal," amesema Pompeo.

Ziara ya kupinga ushawishi wa China Afrika

Ba kwa upande wake amethibitisha wasiwasi ulioko kuhusu ugaidi, na jinsi unavyosambaa kwa kasi Afrika Magharibi. Amesisitiza kwamna  serikali ya Senegal na ya Marekani zinashirikiana kwa karibu kumaliza vitisho kwa amani ya kikanda na ya ulimwengu kama vile ugaidi na uhalifu wa kuvuka mipaka.

"Afrika kwa sasa inatikiswa na mizozo mingi na utulivu hauwezi kupatikana bila Waafrika. Hali inavyoendelea nchini Libya ni mfano mzuri," ameongeza Ba.

Umoja wa Afrika, Addis Ababa, EthiopiaPicha: Getty Images/AFP/M. Tewelde

Baada ya kukamilisha ziara yake Senegal, Pompeo ameondoka na kuelekea Angola na baadaye atakwenda nchini Ethiopia, ikiwa ni mojawapo ya juhudi za kutaka kuzuia ushawishi wa China na Urusi pamoja na mataifa mengine yenye nguvu duniani barani Afrika kwenye idadi kubwa ya vijana wapatao bilioni 1.2.

Akiwa Angola, Pompeo atakutana na rais wa nchi hiyo, Joao Lourenco, anayepambana na sakata la rushwa linalomhusisha mtoto wa kiongozi wa zamani wa nchi hiyo, Isabel dos Santos.

Baada ya hapo, Pompeo ataelekea Ethiopia, taifa la pili barani Afrika lenye idadi kubwa ya watu wapatao milioni 100 na pia ndiko yaliko makau makuu ya Umoja wa Afrika.

Vyanzo: rtre, ap