Pompeo ashambulia sera za Obama mashariki ya kati
11 Januari 2019Aliyasema hayo katika ukosoaji mkubwa wa sera za rais huyo wa zamani licha ya hatua za mkuu wa Pompeo rais Donald Trump kuamua kuviondoa vikosi vya jeshi la Marekani kutoka Syria.
Katika bhotuba ambayo aliitoa katika chuo kikuu cha Marekani mjini Cairo, Pompeo alijitenga na utamaduni wa kidiplomasia wa Marekani wa kuepuka kutangaza hadharani mizozo wa ndani nchini Marekani kwa kumshambulia Obama katika mahali ambapo mtangulizi huyo wa rais Trum alitoa hotuba ya kihistoria yenye lengo la kuimarisha mahusiano na ulimwengu wa Kiislamu. Pompeo ameiwasilisha Marekani kuwa ni nguvu ya kufanya mazuri katika mashariki ya kati, na kudokeza kwamba Obama aliiona Marekani kama " nguvu inayoitaabisha mashariki ya kati".
"Tunahitaji kutambua ukweli huu kwasababu iwapo hatutafanya hivyo, tutafanya makosa ya uchaguzi. Kwa hivi sasa na hapo baadaye. Na uchaguzi wetu , kile tutakachokichagua leo kina athari kwa mataifa na kwa mamilioni ya watu , kwa usalama wetu, kwa ufanisi wa uchumi wetu, kwa uhuru wetu , na ule wa watoto wetu."
Akosolewa
Baadhi ya maafisa wa zamani wa Marekani na wachambuzi wamemshutumu mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Marekani kwa kusoma vibaya historia na kujificha katika mapenzi ya binafsi ya Trump kupunguza jukumu lake katika eneo hilo.
Pompeo amemshutumu Obama kwa kushindwa kupima uwezo na ushupavu wa Uislamu wa itikadi kali," na kushindwa kuunga mkono kile alichokiita vuguvugu la kijani la maandamano ya umma kupinga uchaguzi uliobishaniwa nchini Iran, na kutupia lawama kwa kutoishambulia Syria kwa kulipiza kisasi kwa matumizi ya silaha za sumu ya majeshi ya serikali katika vita vya wenyewe kwa wenyewe .
"Kitu gani tulijifunza kutokana na hali hii ? Tumejifunza kwamba wakati Marekani inajiweka kando, machafuko yanafuatia. Wakati tunawapuuza marafiki, sononeko la chuki vinajijenga. Na wakati tunashirikiana na maadui zetu, wanasonga mbele," Pompeo alisema.
Pompeo hakumtaja Obama kwa jina lakini alimuita "Mmarekani mwingine" ambaye alitoa hotuba katika mji wenye wakaazi wengi katika mataifa ya Kiarabu . Ofisi ya Obama ilikataa kutoa maelezo kuhusu hotuba hii.
Pompeo anafanya ziara katika eneo hilo kujaribu kuelezea mkakati wa Marekani baada ya tangazo la kushangaza la Trump mwezi uliopita la kuwaondoa kwa ghafla wanajeshi 2,000 wa Marekani kutoka Syria, hatua iliyowashangaza washirika, kuwashitua maafisa wa ngazi ya juu wa Marekani na kusababisha kujiuzulu kwa waziri wa ulinzi wa Marekani Jim Mattis.
Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre
Mhariri: Josephat Charo