1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Pompeo atetea mkutano wa Trump na Putin

Isaac Gamba
26 Julai 2018

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Mike Pompeo amemtetea kwa nguvu  Rais Donald Trump kuhusiana na sera yake ya kigeni, wakati mwanadiplomasia huyo  alipohojiwa  na kamati ya mambo ya nje ya seneti.

USA Washington Capitol Hill | Mike Pompeo, Außenminister
Picha: picture-alliance/dpa/CNP/R. Sachs

Hayo yanajiri  huku maseneta  kutoka vyama vya Republican na Democrats wakiendelea kumkosoa  Trump  hususani kwa matamshi yake ya hivi karibuni aliyoyatoa wakati wa mkutano wa kilele kati yake na rais Vladimir Putin wa Urusi ambapo alishindwa kumbana Putin juu ya madai ya kuingilia uchaguzi wa Marekani wa mwaka 2016  na kuonekana  kukubaliana naye hatua iliyoibua mjadala nchini Marekani licha ya Trump kulazimika kufafanua baadaye kuwa aliteleza ulimi na hakumaanisha hivyo.

Rais Vladmir Putin amekuwa akikanusha Urusi kuingilia uchaguzi huo huku Trump naye akisema hakukuwa na makubaliano yoyote juu ya hilo kati ya Marekani na Urusi. Suala hilo kwa sasa liko chini ya kamati ya uchunguzi inayoongozwa na mwanasheria  Robert Mueller.

Kamati hiyo ilizidi kumbana Mike Pompeo  ikisisitiza kupata taarifa juu ya kipi kilichojadiliwa kati ya Trump na Putin wakati viongozi hao walipokuwa peke yao isipokuwa wakalimani  kwa karibu masaa mawili.

Pompeo amesema aliaarifiwa kwa ufasaha kuhusiana na mkutano huo wa ana kwa ana kati ya Trump na rais wa Urusi Vladimir  Putin ambaye mashirika ya kijasusi ya Marekani yanadai kuwa alifahamu juu ya hatua ya Urusi kuingilia uchaguzi wa Marekani mwaka 2016.

Huku akionekana kujikakamua kutoa ufafanuzi  Pompeo alisisitiza kuwa rais ana haki ya kufanya  mikutano ya faragha na kuongeza kuwa hata hivyo  ana fahamu vema kuhusiana na kile kilichojadiliwa wakati huo na viongozi hao wawili.

Seneta Bob Corker Mwenyenyekiti wa Kamati ya Mambo ya nje ya Seneti MarekaniPicha: picture-alliance/AP Photo/E. Schelzig

Seneta Bob Corker  mwenyekiti wa kamati hiyo ya mambo ya nje alimueleza Pompeo kuwa maseneta wana mashaka na utendaji kazi wa ikulu ya Marekani ikiwa ni pamoja na hatua  zinazohusiana na sera za nje za Marekani.

Aliongeza kuwa mashaka hayo yanatokana na kauli za mara kwa mara zinazokanganya zinazotolewa na rais Donald Trump ikiwa ni pamoja na uchunguzi unaoendelea dhidi ya Urusi inayohusishwa na kuingilia uchaguzi wa Marekani mwaka 2016 na matamshi ambayo Trump amekuwa akiyaelekeza dhidi ya nchi washirika.

" Nina imani kubwa na wewe , nadhani wewe ni mzalendo isipokuwa tu matendo ya rais ndio yanaonekana kulifanya taifa letu lisiaminike" aliongeza Corker.

Aidha Corker alihoji juu ya  kauli ya Trump kumsifia  kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un  kuwa ana kipaji kikubwa  na anawapenda watu wake hasa ukichukulia ukiukaji mkubwa dhidi ya haki za binadamu unaofanyika Korea Kaskazini.

Maswali mengine mazito yakiwemo yanayohusu Korea Kaskazini, NATO na Iran nayo pia  yaliulizwa na wajumbe wa kamati hiyo huku Pompeo akisema hapaswi kufichua maudhui ya mazunguzo hayo.

 Mike Pompeo  alifafanua kuwa baadhi ya matamshi ya rais Trump yanazaa matunda  na kutaka utawala wa Marekani kuhukumiwa kwa matendo yake  badala ya matamshi ya rais.

Kwa upande mwingine mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Marekani  akizungmzia suala la Korea Kaskazini  alisema  safari ndefu bado ipo katika mchakato wa kuondoa silaha za nyukilia nchini Korea Kaskazini.

Mwandishi: Isaac Gamba /AFPE/EAP

Mhariri: Iddi Ssessanga

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW